ZANZIBAR.
Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) imesema inaendelea kuwekeza katika kukuza utaalamu wa wahandisi wa ndani na kuimarisha ushirikiano na vyuo vikuu pamoja na taasisi za mafunzo ya ufundi ili kuchochea maendeleo endelevu ya viwanda nchini.
Dhamira hiyo imeelezwa wakati wa Mkutano wa Tisa wa Kimataifa wa Uhandisi wa Mitambo na Viwanda (MIE 2026), uliofanyika katika Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zanzibar, uliowakutanisha watafiti, wahandisi, wanafunzi, viongozi wa viwanda na watunga sera.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhandisi Sandra Suleiman wa EACOP amesema uwekezaji katika programu za kujenga uwezo wa kitaalamu na ushirikiano na taasisi za elimu ni muhimu katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika kuendeleza sekta ya viwanda nchini.
Amesema ushirikiano kati ya viwanda na taasisi za kitaaluma unasaidia kuunganisha maarifa yanayotolewa darasani na mahitaji halisi ya sekta ya viwanda, hivyo kuwawezesha wanafunzi na wataalamu kupata ujuzi unaoendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Mkutano huo, wenye kaulimbiu isemayo “Ubunifu wa Uhandisi kwa Mabadiliko Endelevu ya Viwanda kuelekea Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050,” ulitoa fursa kwa washiriki kujadili teknolojia na suluhisho za kihandisi zinazoweza kuongeza tija, kukuza viwanda na kuimarisha maendeleo endelevu.
Ushiriki wa EACOP umeonesha msisitizo wa kampuni hiyo katika kukuza vipaji vya Watanzania, kuongeza ushiriki wao katika mnyororo wa thamani na kuimarisha ubadilishanaji wa maarifa kati ya sekta ya viwanda na taasisi za mafunzo. Kampuni hiyo imesisitiza kuwa uwekezaji katika watu na ujuzi wa kitaalamu ni muhimu katika kujenga uwezo wa ndani wa kukidhi mahitaji ya viwanda na miundombinu nchini.

Hakuna maoni: