SERIKALI YASISITIZA UHAWILISHAJI TEKNOLOJIA KATIKA MIRADI YA MADINI MKAKATI

📍Bungeni- Dodoma.

Serikali imesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mikataba ya uhawilishaji teknolojia (Technology Transfer Agreements) katika miradi ya madini, hususan madini mkakati (Critical Minerals), ili kuimarisha ujuzi, utaalamu na uwezo wa kiteknolojia wa Watanzania katika sekta ya madini.

Akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini, Mhe. Esther Matiko, kuhusu Sera ya kuimarisha mikataba hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amesema Serikali imeweka misingi ya kisheria inayowataka wawekezaji katika sekta ya madini kushirikiana na wataalamu wazawa katika uhawilishaji wa maarifa na teknolojia.

Amesema Sera ya Madini ya mwaka 2009, hususan Ibara ya 5.12, inasisitiza umuhimu wa kuimarisha ujuzi na uwezo wa kitaalamu wa Watanzania kupitia mafunzo na ushirikiano na kampuni za madini.

Aidha, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa Kifungu cha 135 cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, kinawataka wamiliki wa leseni za madini kuweka utaratibu wa uhawilishaji wa maarifa na teknolojia, kujenga uwezo wa wataalamu wazawa na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa wajibu huo.

Ameongeza kuwa Kanuni za Madini za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018, hususan Kanuni za 27 hadi 29, zinaweka matakwa kwa wawekezaji kuandaa mipango ya uhawilishaji teknolojia na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Tume ya Madini.

Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango hiyo ili kuhakikisha uhawilishaji wa teknolojia unaleta matokeo halisi katika kujenga uwezo wa kitaalamu na kiteknolojia kwa Watanzania.

Amesema hatua hiyo ni muhimu zaidi katika miradi ya madini mkakati, ambayo ina nafasi kubwa katika kukuza viwanda, kuongeza thamani ya madini nchini na kuimarisha manufaa ya rasilimali hizo kwa uchumi wa Taifa.

Kupitia utekelezaji madhubuti wa mikataba hiyo, Serikali inalenga kuhakikisha kuwa uwekezaji katika sekta ya madini hauishii katika uzalishaji wa madini pekee, bali pia unaacha urithi wa maarifa, ujuzi na teknolojia utakaosaidia kukuza uwezo wa wazawa na kuchochea maendeleo endelevu ya sekta hiyo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.