WATANZANIA WAASWA KUJIFUNZA KWA TAMISA KUWEKEZA KATIKA MADINI

DAR ES SALAAM

Na Christopher Siwingwa

Watanzania wamehimizwa kujifunza fursa za uwekezaji katika sekta ya madini kupitia Chama cha Wasambazaji wa Vifaa vya Madini (TAMISA), ili kuongeza ushiriki wao katika biashara ya vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji.

Wito huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa TAMISA, Japhet Mussa, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya vifaa na bidhaa za uchimbaji madini yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Mussa amesema Watanzania hawapaswi kukatishwa tamaa na uwepo wa wawekezaji wa nje wanaomiliki biashara za vifaa vya madini, bali wanapaswa kuona hali hiyo kama fursa ya kujifunza na kuongeza uwezo wao wa kuwekeza katika sekta hiyo.

Ameshauri wawekezaji wadogo wenye mitaji midogo kuungana na wawekezaji kutoka nje ya nchi ili kujifunza mbinu za uwekezaji, kukuza biashara zao na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya sekta ya madini.

Aidha, amesema kuna eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 127 mkoani Geita ambalo Watanzania na wawekezaji wa nje wanakaribishwa kuwekeza katika shughuli za madini, hatua inayolenga kuongeza kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Ameeleza kuwa thamani ya vifaa vinavyoagizwa kutoka nje kwa ajili ya sekta ya madini inazidi Sh trilioni 5.3, akibainisha kuwa uzalishaji wa vifaa hivyo nchini ungeongeza fursa za biashara kwa wazawa na kuchochea ukuaji wa pato la taifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.