Vijana nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya viumbe maji, ikiwamo ufugaji wa samaki, kutokana na uwezo wake wa kuleta faida kwa muda mfupi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa vijana.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Biashara na Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika Ofisi ya Rais, Tume ya Taifa ya Mipango, Bw. Hopeness Kweka, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa sekta binafsi kujadili na kutoa maoni kuhusu maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2027/28.
Kweka amesema sekta binafsi ina mchango muhimu katika maandalizi ya mpango huo, ambapo imepewa nafasi ya kushiriki kwa asilimia 62.5, hatua inayodhihirisha umuhimu wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini.
Amesema maeneo yaliyopewa kipaumbele katika ushiriki huo ni pamoja na uzalishaji wa mafuta ya kula, ufugaji wa viumbe maji, kilimo cha pamba, uzalishaji wa mazao ya nguo, pamoja na utengenezaji wa magari na vipuri vyake.
“Serikali imezichagua sekta hizo kwa malengo mahususi ili kukimbiza umaskini uliopitiliza kwa Watanzania,” alisema Kweka.
Ameeleza kuwa uwekezaji katika maeneo hayo unalenga kuongeza uzalishaji, kutengeneza ajira kwa Watanzania na kupunguza umaskini katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, huku akiwahimiza vijana kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake, Revival Herman, mshiriki kutoka taasisi ya Maritime Empowerment Organisation (MEO), amesema baadhi ya vijana wanakwamishwa na makundi yanayokatishana tamaa kuhusu fursa zinazotolewa na Serikali.
Herman amewataka vijana kujiamini, kuwa wabunifu na kuchukua hatua za kutafuta fursa badala ya kusubiri au kuruhusu maneno ya kukatishana tamaa kuwazuia kufikia malengo yao.
“Ifike wakati kijana ujiamini. Usisubiri kusikia kuna kitu gani; nyanyuka, tafuta fursa,” alisema Herman.
Ameongeza kuwa vijana wanaweza kupata taarifa kuhusu fursa mbalimbali kupitia wenyeviti wa vijiji na halmashauri za wilaya, hivyo kuwataka kutumia mifumo hiyo kutafuta taarifa na kujua namna ya kunufaika na fursa zinazopatikana.

Hakuna maoni: