JESCA KITAMBAA CHEUPE AUNGANISHAJI BURUDANI NA FURSA ZA VIJANA CHIMBO LA VIJANA BRANCH 2026

DAR ES SALAAM. 

Mfanyabiashara na mjasiriamali maarufu jijini Dar es Salaam, Jessica Boniface Kikumbi, maarufu kama Jesca Kitambaa Cheupe, amezindua hafla ya Chimbo la Vijana Branch 2026, inayotarajiwa kuwakutanisha vijana na wananchi kwa siku mbili za burudani, muziki na huduma mbalimbali za kijamii.

Hafla hiyo itafanyika katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 24 hadi 25, 2026, ikiwa na burudani kutoka kwa ma-DJ na wasanii mbalimbali, sambamba na fursa za kujifunza kuhusu ajira, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jesca, ambaye ni mmiliki wa kumbi za burudani na baa za Kitambaa Cheupe nchini, amesema hafla hiyo imeandaliwa kuwakutanisha wananchi katika eneo moja watakapoweza kupata burudani, huduma za kijamii na elimu kuhusu fursa mbalimbali.

Amesema lengo ni kuwapa vijana na wananchi nafasi ya kufurahia burudani huku wakipata maarifa yanayoweza kuwasaidia kuboresha maisha yao, badala ya kutumia muda na gharama kutafuta huduma hizo katika maeneo tofauti.

Mbali na muziki na burudani zitakazotolewa katika siku zote mbili, washiriki watapata fursa ya kufurahia huduma ya supu ya bure kuanzia asubuhi, ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizoandaliwa kuwavutia wananchi kushiriki katika hafla hiyo.

Chimbo la Vijana Branch 2026 pia itakuwa jukwaa la kukutana na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma muhimu kwa wananchi, zikiwemo Bodi ya Mikopo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani, pamoja na taasisi za bima na watoa huduma za afya.

Kupitia taasisi hizo, vijana na wananchi watapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata elimu kuhusu kodi, mikopo, nyaraka za kisheria, bima, afya na uwekezaji, huku wakifurahia burudani zitakazopamba hafla hiyo.

Aidha, ushiriki wa taasisi zinazohusika na uwekezaji unatarajiwa kuwasaidia vijana kufahamu fursa zilizopo na namna ya kuzitumia kuanzisha au kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Kwa kuunganisha muziki, wasanii, huduma ya supu ya bure na huduma za kijamii, Chimbo la Vijana Branch 2026 inatarajiwa kuwa sehemu ya kukutana, kujumuika na kufurahia burudani huku vijana wakipata maarifa na fursa zinazoweza kuchangia maendeleo yao.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.