Dodoma.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kuchukua hatua za kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino ikiwemo kufanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara na madaraja, kubaini maeneo hatarishi na kuimarisha mifereji ya maji ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara wakati wa mvua.
Hatua hizo zinakuja kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuhusu matarajio ya mvua hizo ambapo TARURA imewataka Mameneja wake katika mikoa yote nchini kuendelea kuchukua hatua na kufanya marekebisho ya miundombinu inayohitaji matengenezo kabla ya mvua hizo hazijaanza kunyesha.
Akizungumzia maandalizi hayo, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema Wakala huo tayari umepokea taarifa za maeneo hatarishi kutoka kwa Mameneja wa mikoa na kutoa idhini ya utekelezaji wa matengenezo kwa kutumia bajeti zilizopo.
Amesema maeneo yanayohitaji matengenezo makubwa yanayozidi uwezo wa bajeti zilizopo yanatakiwa kuwasilishwa TARURA Makao Makuu ili maombi ya fedha yaandaliwe na kuwasilishwa serikalini kwa ajili ya kupata rasilimali fedha za ziada.
"Kwa sasa kazi za mifereji zinaendelea lakini ninatoa msisitizo kwa mameneja kuhakikisha ukaguzi wa barabara, madaraja na maeneo hatarishi unaendelea, ni muhimu kusafisha mifereji na kuondoa vifusi vilivyowekwa pembeni ya mifereji ili mvua zitakaponyesha maji yaweze kupita kwa urahisi bila kusababisha mafuriko au uharibifu wa miundombinu", amesema.
Mhandisi Seff amewataka wananchi kushirikiana na TARURA kwa kutoa taarifa za haraka pindi watakapobaini kuharibika kwa barabara, madaraja au miundombinu mingine inayoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji.
Amesema wananchi wanaweza kuwasilisha taarifa hizo katika ofisi za TARURA zilizopo wilayani na mikoani kupitia namba za simu za bure zinazopatikana katika kila mkoa ili kuwezesha Wakala kuchukua hatua za haraka kulingana na ukubwa wa tatizo litakalojitokeza.
Ameongeza kuwa pale ambapo miundombinu itakuwa katika hali inayohatarisha usalama, TARURA itaweka tahadhari kwa umma au kufunga kwa muda eneo husika kutegemeana na ukubwa wa uharibifu ili kuzuia ajali na kulinda maisha ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Seff amewashauri wananchi kuepuka safari zisizo za lazima wakati wa mvua kubwa na kusubiri mvua ipite kabla ya kuendelea na safari huku wakihakikisha njia wanazotumia ni salama.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuepuka kujaribu kuvuka maeneo yenye mafuriko, madaraja yaliyofunikwa na maji au sehemu ambazo usalama wake haujathibitishwa kwani kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha maisha yao.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika kulinda na kutunza miundombinu inayojengwa na kukarabatiwa na serikali ikiwemo madaraja, alama za barabarani na mifereji ya maji kwa kuwa miundombinu hiyo ni mali ya umma inayopaswa kutunzwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, Mhandisi Seff amesema TARURA inaendelea kutekeleza Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (CBRM) unaowashirikisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na barabara husika.
Kupitia mpango huo, wananchi hupewa mafunzo ya kuanzisha vikundi vya kijamii na kushiriki katika kazi za matengenezo ya kawaida ya barabara ikiwemo kufyeka nyasi, kusafisha mifereji na kufanya shughuli nyingine zinazosaidia kudumisha ubora na matumizi ya barabara.
Amesema ushiriki huo unalenga kuwapa wananchi nafasi ya kuchangia moja kwa moja katika utunzaji wa miundombinu inayowahudumia huku ukiimarisha ushirikiano kati ya TARURA na jamii katika kuhakikisha barabara zinaendelea kupitika kwa usalama.
"Tunawaomba wananchi washirikiane na wataalamu wetu wanapofika kutoa elimu kuhusu mpango wa CBRM na pale vikundi vinapopewa kazi vihakikishe kazi zinatekelezwa kwa ufanisi", amesisitiza Mhandisi Seff.
TARURA imeendelea kusisitiza ushirikiano wa wananchi katika utoaji wa taarifa kwa wakati ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa ili kulinda maisha ya watu na kuhakikisha miundombinu ya barabara inaendelea kutoa huduma kwa usalama.

Hakuna maoni: