DAR ES SALAAM.
Mfuko wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha (SELF Microfinance Fund) umepata faida ya shilingi bilioni 3.19 na kutoa gawio la shilingi milioni 490 kwa Serikali katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2023 hadi 2026.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Ofisa Mtendaji Mkuu wa mfuko huo, Santiel Yona, amesema taasisi hiyo imeendelea kutoa mikopo kwa wakulima, wavuvi, vijana, wafanyabiashara na watumishi wa umma ili kuwawezesha kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Yona amesema huduma za mikopo hutolewa kupitia taasisi na vyama vya kifedha vinavyowakopesha wananchi, pamoja na mikopo inayotolewa moja kwa moja kwa walengwa. Ameeleza kuwa huduma hizo zimechangia upatikanaji wa ajira 262,624, huku akisisitiza umuhimu wa mikopo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Amesema mbali na mikopo, SELF Microfinance Fund hutoa elimu ya fedha kuhusu masharti ya mikopo, viwango vya riba na taratibu za marejesho ili kuwasaidia wateja kutumia fedha kwa ufanisi. Taasisi hiyo pia hutoa huduma za bima na kubuni bidhaa maalumu za mikopo kwa vijana wanaotaka kujiajiri kupitia usafiri wa bajaji na wananchi wanaohitaji nishati safi.
Kwa mujibu wa Yona, taasisi hiyo kwa sasa ina matawi 12 na vituo viwili vya huduma, huku ikiendelea kuweka mikakati ya kupanua wigo wa kuwafikia wananchi kupitia huduma za kidijitali
Hata hivyo, amesema mfuko huo unakabiliwa na changamoto za uelewa mdogo wa elimu ya fedha, baadhi ya wakopaji kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati na changamoto zinazohusiana na biashara zisizo rasmi. Amesema wataendelea kutoa elimu kwa wateja na kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine ili kuimarisha huduma za kifedha, kuongeza ajira na kukuza kipato cha wananchi.



Hakuna maoni: