TANZANIA YATANGAZA UTALII WA MADINI QATAR

Doha, Qatar

Tanzania imetangaza fursa na vivutio vya utalii wa madini nchini Qatar, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza sekta hiyo, kuongeza idadi ya watalii na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ameongoza ujumbe wa Tanzania nchini Qatar, ambapo amefanya mazungumzo na viongozi na wadau wa sekta ya utalii nchini humo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar katika kukuza utalii, hususan utalii unaohusisha vivutio vya madini.

Akizungumza baada ya kutembelea na kufanya mazungumzo na uongozi wa utalii nchini Qatar, Dkt. Kiruswa amesema Tanzania ina fursa kubwa katika sekta ya utalii kutokana na kuwa na vivutio mbalimbali, ikiwemo utalii wa madini, mbuga za wanyama, bahari na fukwe pamoja na vivutio vilivyopo Zanzibar.

Amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na Qatar katika kuendeleza, kutangaza na kuvutia watalii katika vivutio vilivyopo nchini, hatua ambayo itasaidia kuongeza mapato, ajira na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, ikiwemo utalii wa madini, wanyamapori, bahari na Zanzibar. Tunataka kutumia fursa hii kuimarisha ushirikiano na Qatar ili kutangaza vivutio vyetu na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania,” amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Mohamed, ameupongeza uongozi wa utalii wa Qatar kwa kukubali kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi hizo.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza uelewa kuhusu fursa za utalii zilizopo Tanzania na Qatar, sambamba na kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi hizo.

Naye, Mwenyekiti wa Utalii nchini Qatar, Saad Bin Ali AlKharji ameipongeza Tanzania kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Qatar katika kukuza utalii wa madini na sekta nyingine za utalii.

Ameahidi kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika kuhakikisha vivutio vya utalii, ikiwemo utalii wa madini, vinatangazwa kwa kiwango kikubwa nchini Qatar ili kuvutia watalii zaidi kutembelea Tanzania.

Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa zaidi za kutangaza utalii wa madini wa Tanzania katika masoko ya kimataifa, pamoja na kuchochea uwekezaji na shughuli nyingine za kiuchumi zinazohusiana na sekta ya utalii.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.