TBA YATANGAZA VIWANJA VYA UWEKEZAJI GEITA, YALENGA UJENZI WA GHOROFA ZA MAKAZI

Na Mwandishi Wetu,

Geita.

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya majengo nchini, ukiwemo ujenzi wa majengo ya makazi ya ghorofa katika eneo la Bishota mkoani Geita, pamoja na maeneo mengine 38 yaliyopo Tanzania Bara yanayolengwa kuvutia wawekezaji kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo Leo Oktoba 2,2026 wakati wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Katika Viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan Mkoani Geita ,Meneja Mawasiliano na Masoko wa TBA, Adam Mwingira, amesema hayo wakati akielezea fursa za uwekezaji zilizowasilishwa na wakala huo katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.

Mwingira amesema Geita ina maeneo mawili yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji, yakiwemo Bishota na Msigiti, ambayo yanatarajiwa kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika miradi mbalimbali ya ujenzi.

Amesema katika eneo la Bishota, TBA inapanga kujenga majengo ya makazi yenye jumla ya nyumba 12, yatakayokuwa na takribani ghorofa sita, huku nyumba hizo zikiwa na vyumba vya kulala kimoja, viwili na vitatu ili kukidhi mahitaji ya makundi tofauti ya wakazi.

Ameeleza kuwa mpango huo ni sehemu ya jitihada za wakala huo kutangaza maeneo yenye fursa za uwekezaji na kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza miradi ya majengo kupitia mfumo wa PPP.

Kwa mujibu wa Mwingira, mbali na maeneo ya Geita, TBA inaendelea kutangaza maeneo mengine 38 yaliyopo Tanzania Bara kwa lengo la kuyafanya yavutie wawekezaji na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya miundombinu ya majengo nchini.

Katika hatua nyingine, Mwingira amesema TBA inaendelea kutekeleza majukumu yake ya ujenzi wa majengo ya umma, makazi ya watumishi na miundombinu mingine inayohitajika na Serikali pamoja na wananchi.

Amezitaja hospitali za Chato na Geita kuwa miongoni mwa miradi ya afya iliyotekelezwa na wakala huo, huku akieleza kuwa taasisi hiyo pia imejenga nyumba za viongozi wa Serikali, ikiwemo nyumba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita iliyokamilika.

Aidha, amesema TBA imeshiriki katika miradi ya makazi ya Magomeni jijini Dar es Salaam, ambako awamu ya kwanza ya nyumba imekamilika na kuanza kutumiwa na wakazi, huku ujenzi wa awamu nyingine ukiendelea.

Mwingira ameongeza kuwa wakala huo pia hutoa huduma za kitaalamu katika miradi ya Serikali, ikiwemo usanifu na usimamizi wa ujenzi wa majengo, akitolea mfano jengo la Serikali lililopo Chamwino.

Akizungumzia ushiriki wa TBA katika maonesho hayo, Mwingira amesema wakala huo umepata nafasi ya pili katika kundi la taasisi za umma zilizoshiriki, akiwashukuru wadau waliotembelea banda lake na kufuatilia shughuli zake kupitia mitandao ya kijamii.

Amesema tuzo hiyo ni matokeo ya ushiriki wa wadau pamoja na ushirikiano wa uongozi na watumishi wa taasisi hiyo katika kuwasilisha huduma na fursa zinazotolewa na TBA.

Amehimiza wawekezaji na wadau wenye nia ya kushiriki katika miradi ya majengo kuendelea kufuatilia taarifa za wakala huo kupitia njia zake rasmi za mawasiliano ili kupata maelezo kuhusu maeneo na miradi inayotangazwa.

Fursa hizo zinakuja wakati maonesho ya teknolojia ya madini mjini Geita yakiwakutanisha wadau wa sekta mbalimbali, yakitoa nafasi kwa taasisi za umma kutangaza huduma zao na kutafuta ushirikiano wa uwekezaji unaoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.