DCEA YA SHINDA TUZO YA UBORA WA TAARIFA ZA HESABU KWA MARA YA TISA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea kuimarisha rekodi yake katika usimamizi wa fedha za umma baada ya kushinda tuzo ya kwanza ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, katika kundi la taasisi za Serikali zinazojitegemea.

Tuzo hiyo iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), inatambua taasisi zinazozingatia ubora na Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS) wakati wa kuandaa taarifa za hesabu.

Akizungumzia mafanikio hayo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema ushindi huo ni uthibitisho wa weledi, uwajibikaji na usimamizi bora wa fedha za umma ndani ya mamlaka hiyo.

Amesema DCEA inaendelea kuhakikisha rasilimali inazopatiwa zinasimamiwa kwa uadilifu na uwazi ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

Aidha, amewapongeza watumishi wote wa mamlaka hiyo, hususan wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu pamoja na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, kwa ushirikiano na kujituma vilivyochangia kupatikana kwa tuzo hiyo.

Kwa mujibu wa DCEA, ushindi huo ni wa mara ya tisa kwa mamlaka hiyo kupata tuzo za NBAA tangu mwaka 2017, huku ikiendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha, uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.