NYWELE ZAFUNGUA UKURASA MPYA WA UZALISHAJI WA MBOLEA TANZANIA

DODOMA.

Ubunifu wa kutumia taka za nywele za binadamu kuzalisha mbolea na virutubisho vya mimea unatajwa kuwa miongoni mwa suluhisho linaloweza kuongeza upatikanaji wa pembejeo nchini, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kutoa thamani ya kiuchumi kwa taka ambazo awali zilikuwa zikitupwa au kuchomwa.

Mjasiriamali kijana David Denis, mwanzilishi wa kampuni ya CutOff Recycle Limited, amesema ubunifu huo ulianza mwaka 2017 hadi 2018 alipokuwa akisoma kidato cha tano na sita, akiwa na ndoto ya kuwa daktari kama ilivyokuwa matarajio ya familia yake.

Amesema wazo la kutumia nywele kutengeneza mbolea lilimjia baada ya kwenda kunyolewa saluni na kugundua kuwa nywele nyingi zilizokuwa zikikatwa zilitupwa au kuchomwa. Alipofuatilia zaidi, alikumbuka maelezo aliyoyasoma katika ukurasa wa 78 wa kitabu cha Biological Science kuhusu protini na muundo wa amino acid unaopatikana katika nywele za binadamu.

Denis amesema utafiti zaidi ulimwezesha kubaini kuwa nywele zina kiwango kikubwa cha naitrojeni (Nitrogen), kirutubisho muhimu kwa ukuaji wa mimea, jambo lililomshawishi kuachana na ndoto ya udaktari na kujikita katika utafiti na uzalishaji wa mbolea. Ameeleza kuwa licha ya taka hizo kutumika kutengeneza bidhaa katika sekta nyingine, ikiwemo uhandisi wa ujenzi, fursa yake katika kilimo ilikuwa bado haijatumika kikamilifu.

Akielezea fursa ya soko iliyomvutia kuingia katika uzalishaji huo, amesema wakati anaanza ubunifu huo alibaini kuwa zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji ya mbolea nchini yalitoka nje ya nchi, huku asilimia 10 iliyozalishwa ndani ikiwa na asilimia 80 ya uzalishaji wake ukifanywa na kampuni moja pekee.

Amesema kampuni yake imeendelea kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo mbolea ya majimaji yenye amino acid, mbolea hai na virutubisho vya mimea, ambazo zimefanyiwa vipimo katika maabara ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA). Kwa mujibu wake, sampuli ya mbolea ya majimaji ilionyesha jumla ya asilimia 4.06 ya virutubisho vya naitrojeni, fosforasi na potasiamu (NPK), kiwango kinachozidi kiwango cha chini cha asilimia tatu kinachotakiwa kwa mujibu wa viwango husika vya Afrika Mashariki.

Aidha, amesema teknolojia hiyo imefanikiwa kupata hati miliki yenye namba TZ/P/2024/00036 iliyotolewa Septemba 18, 2024, inayolinda teknolojia ya kuzalisha mbolea ya majimaji yenye amino acid kutokana na taka za nywele za binadamu. Kampuni hiyo pia imepanua wigo wa bidhaa zake kupitia bidhaa za Rutubisha, McheKuza na Vuna, huku ikiwa imewasilisha maombi ya hati miliki ya kimataifa mwaka 2026 kwa mfumo wa usambazaji wa mbolea unaotumia teknolojia ya akili mnemba (AI).

Akizungumzia changamoto zinazoikabili sekta hiyo, Denis amesema mitaji na gharama za taratibu za udhibiti zimeendelea kuwa vikwazo vikubwa. Amesema licha ya ushirikiano kati ya wajasiriamali na mamlaka za udhibiti kuimarika, gharama za kupata ithibati bado ni kubwa, akitolea mfano ada ya dola za Marekani 10,000 kwa ajili ya kipimo cha ufanisi wa bidhaa (Efficacy Test), hali inayowakwamisha wajasiriamali wadogo na wa kati.

Kuhusu upanuzi wa uzalishaji, amesema kampuni imekua kutoka kiwanda kidogo hadi hatua ya kujenga kiwanda kikubwa eneo la Dakawa, mkoani Morogoro, chenye ukubwa wa zaidi ya futi za mraba 1,000 na eneo la zaidi ya ekari 20 linaloandaliwa kwa shughuli za uzalishaji. Ameeleza kuwa wanatarajia kukamilisha ufungaji wa laini ya uzalishaji ifikapo mwishoni mwa Januari 2027, ikiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni moja za mbolea ya maji kwa mwaka pamoja na tani 100,000 za mbolea za mboji.

Ameongeza kuwa kwa sasa kampuni inaendesha uzalishaji katika kiwanda kilichopo SIDO jijini Arusha, chenye uwezo wa kuzalisha tani tano za mbolea ya mboji kwa wiki, sawa na takribani tani 200 kwa mwakana tani 12,000 kwa mwaka.

Denis amesema kampuni inakusanya taka za nywele kutoka Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha, ambapo watu wanaokusanya na kuzipeleka katika vituo vya kampuni hulipwa Sh300 kwa kila kilo.Hata hivyo, mahitaji yameendelea kuwa makubwa kuliko uwezo wa uzalishaji hali iliyowalazimu kufikiria kupanua kiwanda chao na kuongeza uzaishaji ili kukidhi mahitaji ya soko.

Akielezea matokeo ya matumizi ya bidhaa hizo, amesema baadhi ya wakulima wameripoti kunufaika, akiwemo mkulima wa mahindi kutoka Mbeya aliyeripoti ongezeko la mavuno kwa takribani asilimia 40 ikilinganishwa na msimu uliopita, pamoja na wakulima wa maua na nyanya na mboga kutoka Arusha.

Kutokana na changamoto zilizopo katika sekta ya uzalisha mbolea ameimba Serikali kupitia upya sera na sheria zinazohusu sekta ya pembejeo ili ziwe rafiki kwa vijana na wajasiriamali wadogo, ikiwemo kuangalia upya au kuondoa baadhi ya ada zinazotozwa kwa dola za Marekani. Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya viwanda na maeneo maalumu ya uzalishaji ili kuwawezesha wabunifu kuhamisha teknolojia zao kutoka hatua ya mawazo na majaribio na kuwa halisi n hatimae kwenda katika uzalishaji wa kibiashara.

Denis ameeleza hayo wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Wadau wa Pembejeo Hai za Kilimo Ikolojia Tanzania 2026, uliofanyika Dodom kuanzia novemba 26-27 jijini Dodoma, ambapo mkutano huo umeandaiwa na Shirika la Iles de Paix, uliowakutanisha wadau kujadili fursa, changamoto na namna ya kuimarisha uzalishaji na Matumizi ya pembejeo hai nchini.




Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.