DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo utafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere na unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki 1,700 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wawakilishi wa kampuni mbalimbali zinazojihusisha na shughuli za madini.
Akitoa taarifa kuhusu mkutano huo Novemba 17, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema sekta ya madini imeendelea kuimarika kutokana na juhudi za Serikali katika kuboresha usimamizi wa rasilimali, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kuvutia uwekezaji na kuwawezesha wachimbaji wadogo.
Mavunde amesema mapato ya Serikali yatokanayo na sekta hiyo yameongezeka kutoka Sh526 bilioni katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Sh1.39 trilioni mwaka 2025/2026. Pia, mchango wa madini katika pato la Taifa ulipanda kutoka asilimia 7.8 mwaka 2024 hadi asilimia 10.3 mwaka 2025.
Ameongeza kuwa thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi iliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi bilioni 5.46 mwaka 2025, huku ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani katika sekta hiyo ukipanda kutoka Sh884.09 bilioni mwaka 2010 hadi Sh5.2 trilioni mwaka 2025.
Katika eneo la ajira, amesema sekta hiyo ilikuwa na ajira rasmi 10,874 hadi Aprili 2025, ambapo asilimia 97.4 zilikuwa za Watanzania. Mkutano huo ulioanzishwa mwaka 2019, mwaka huu utaendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo, “Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuufunga mkutano huo, huku Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akiwa mgeni rasmi katika hafla ya Usiku wa Madini.


Hakuna maoni: