Dar es Salaam, Novemba 17, 2026.
Waandishi wa habari 64 pamoja na vyombo vya habari 11 wamefanikiwa kuingia hatua ya mwisho ya kuwania Tuzo za Uandishi wa Habari za Maendeleo (Samia Kalamu Awards 2026), baada ya kukamilika kwa mchakato wa tathmini uliohusisha kazi 3,003 zilizowasilishwa mwaka huu.
Orodha ya waliofuzu imetangazwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Rolf Kibaja, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Peter Mwasyalanda, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za TCRA.
Kibaja amesema kati ya kazi 3,003 zilizowasilishwa, jumla ya kazi 882 zilifuzu kuingia hatua ya kupigiwa kura na wananchi, ambapo kura 317,399 zilipigwa. Ameeleza kuwa waliopenya hadi hatua ya mwisho wamepatikana kupitia tathmini ya majaji 19 pamoja na ushiriki wa wananchi katika mchakato huo.
Amesema tathmini ya majaji ilizingatia ubora wa maudhui, uzingatiaji wa maadili ya taaluma, matumizi ya tafiti na takwimu, athari chanya kwa jamii pamoja na mchango wa kazi husika katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Washindi wa msimu wa pili wa tuzo hizo wanatarajiwa kutangazwa na kutunukiwa Desemba 5, 2026, katika hafla itakayofanyika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Tuzo hizo zinaratibiwa na TCRA kwa kushirikiana na TAMWA na JAB, zilianzishwa mwaka 2024 na hafla ya kwanza kufanyika mwaka 2025, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Kalamu kwa Maendeleo.”





Hakuna maoni: