DRC YAVUTIWA NA MFUMO WA TANZANIA KUWAENDELEZA WACHIMBAJI WADOGO

Dodoma.

Uzoefu wa Tanzania katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini umevutia Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FESOCOMIC), ambalo limetuma ujumbe wa watu 17 nchini kujifunza mifumo inayotumika kukuza sekta hiyo.

Mwenyekiti wa FESOCOMIC, Alex Murusi, amesema ziara hiyo imetokana na kuvutiwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo, kusimamia masoko ya madini, kudhibiti utoroshaji na kuwawezesha wachimbaji kupata mikopo na ruzuku.

Akizungumza Novemba 3, 2026, Murusi amesema wameona Tanzania ikiweka mipango ya muda mrefu inayolenga kuongeza uwezo wa wachimbaji wadogo kiuchumi na kiteknolojia, ikiwemo kuimarisha utafiti wa kina wa madini ili kuwawezesha kupata taarifa muhimu za maeneo ya uchimbaji. Amesema juhudi hizo zimeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.

Ujumbe huo pia umepongeza Wizara ya Madini na taasisi zake, zikiwemo Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), kwa mipango ya utafiti, mafunzo na utoaji wa leseni za uchimbaji mdogo. Pia umevutiwa na utoaji wa mitambo 15 ya uchorongaji kwa vijana na wanawake kupitia Programu Maalumu ya MBT.

Akielezea maendeleo ya sekta hiyo, Kamishna Msaidizi wa Madini anayesimamia Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Terence Ngole, amesema mchango wa wachimbaji wadogo katika maduhuli yatokanayo na sekta ya madini umeongezeka na kufikia asilimia 40. Ameongeza kuwa sekta nzima ya madini inachangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa DRC umeonyesha kuvutiwa na mifumo ya masoko na vituo vya ununuzi wa madini, hatua ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kununua tani 35 za dhahabu na juhudi za Serikali kuwezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo.

Ujumbe huo pia umepangiwa kutembelea miradi ya uchimbaji, vituo vya uchenjuaji na viwanda vya uongezaji thamani ya madini ili kujifunza kwa vitendo namna mifumo hiyo inavyofanya kazi katika mnyororo mzima wa thamani wa madini nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.