WANANCHI ZAIDI YA MILIONI 30 WANUFAIKA NA UPANUZI WA MAWASILIANO NCHINI


Dar es Salaam.

Zaidi ya wananchi milioni 30 nchini tayari wananufaika na huduma za mawasiliano ya simu kupitia miradi ya ujenzi wa minara inayotekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), huku juhudi za kuwafikia wananchi wengine zikiendelea katika maeneo mbalimbali.

Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Albert Richard, amesema hadi Septemba 2026 huduma hizo zilikuwa zimefika katika kata 2,053 zenye vijiji 5,185, kupitia minara 2,199 iliyokamilika na kuwafikia wananchi 30,051,214.

Amesema mfuko huo umeingia mikataba ya ujenzi wa minara 2,324 katika kata 2,306 zenye vijiji 5,505, huku kazi zikiendelea katika kata 253 na vijiji 320 ambako minara 251 inajengwa. Miradi hiyo inatarajiwa kuongeza idadi ya wananchi watakaopata huduma za mawasiliano hadi 32,789,590, kwa gharama ya jumla ya Sh bilioni 374.

Albert amebainisha kuwa tangu mwaka 2012, UCSAF imetekeleza miradi ya ujenzi wa minara katika awamu 21, ikiwemo minara 758 iliyokamilika kwa gharama ya Sh bilioni 126 na kufikisha huduma kwa wananchi wapatao milioni 8.5. Kwa sasa mfuko huo unaendelea na mradi mwingine wa minara 287 unaogharimu Sh bilioni 29.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Novemba 3, 2026, katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Richard amesema UCSAF pia inaandaa mpango wa kuboresha mawasiliano katika reli ya kisasa ya SGR ili abiria wanaosafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma waweze kupata huduma ya mtandao wakati wote wa safari.

Katika hatua nyingine, amesema mfuko huo unakabiliwa na changamoto ya gharama za uendeshaji wa huduma ya intaneti ya bure katika maeneo ya wazi (Public WiFi), hasa baada ya kukamilika kwa uwekaji wa miundombinu.

 Amesema mradi huo ulianza mwaka wa fedha 2024/25 na ulikuwa na mpango wa kufikisha huduma katika maeneo 60 Tanzania Bara na Zanzibar mwaka wa fedha 2025/26, huku mfumo wa kuwapa watumiaji muda wa awali bila malipo kabla ya kuendelea kwa malipo ukiendelea kutafutwa.

Richard ameongeza kuwa UCSAF inaendelea kuboresha huduma za utangazaji kwa kujenga vituo 37 vya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa gharama ya Sh bilioni 15.5, pamoja na mradi wa redio za jamii katika maeneo zaidi ya 15 unaohusisha ujenzi wa minara na studio kwa gharama ya Sh bilioni sita. 

Katika sekta ya elimu, zaidi ya shule 1,167 zimefaidika na vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya takribani Sh bilioni 17.7, huku shule 22 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu zikipatiwa vifaa vya elimu ya kidijitali.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Msajili wa Hazina, Sabatho Kosuli, amesema UCSAF ni taasisi muhimu katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii kupitia upatikanaji wa huduma za mawasiliano zinazofungua fursa za ajira, biashara na uchumi wa kidijitali.

Aidha  Amewataka waandishi wa habari kuelimisha wananchi kuhusu miradi hiyo na mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.