Sumbawanga, Rukwa.
Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa inaendelea kuboresha miundombinu ya usafiri kupitia mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 60.7, sawa na asilimia 98 ya barabara zote za lami zenye urefu wa kilomita 62 zilizopo mkoani humo.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Chacha Mwita Moseti, amesema hali ya barabara katika Manispaa ya Sumbawanga ni nzuri, huku uwepo wa taa katika barabara hizo ukirahisisha usafiri na kuongeza usalama kwa watumiaji nyakati za usiku na mchana.
Amesema mtandao huo umeongeza urahisi wa kufikika kwa huduma muhimu za kijamii na kiuchumi zikiwemo afya, elimu na masoko, hasa katika maeneo ambayo awali yalikuwa na changamoto ya kufikika. Ameongeza kuwa barabara hizo zimechangia kuboresha mandhari ya mji na kurahisisha shughuli za wananchi.
Akizungumzia hali ya barabara kwa Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, Moseti amesema asilimia 72.4 ya mtandao wa barabara zinapitika na kwamba TARURA inaendelea na matengenezo. Kwa mwaka wa fedha 2026/27, wakala huo umetengewa bajeti ya Sh bilioni 12.4, ambapo tayari umekamilisha manunuzi ya asilimia 60 na wakandarasi wameanza utekelezaji wa kazi katika maeneo mbalimbali.
Kuhusu maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Niño, Moseti amesema wamezibua mitaro, kusafisha mito na kubaini maeneo hatarishi ili kuhakikisha maji yanapita bila vikwazo na kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa endapo changamoto zitatokea.
Kwa upande wake, Juma Abubakar Juma, dereva wa bajaji na mkazi wa Majengo, amesema barabara za lami zimemrahisishia shughuli za kusafirisha abiria, huku gharama za matengenezo ya chombo chake zikipungua. Naye Salafina Kilapi, mkazi wa eneo hilo, amesema ujenzi wa barabara hizo umeboresha usafiri na kuongeza usalama kutokana na uwepo wa taa za barabarani.





Hakuna maoni: