TISEZA YAIBUA FURSA MPYA ZA AJIRA KUPITIA UWEKEZAJI WA DOLA BILIONI 15.32

DAR ES SALAAM.

Uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 15.32 uliosajiliwa nchini unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 344,000, kufuatia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kusajili miradi 1,148 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Septemba 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead John Teri, amesema hayo Novemba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).

Amesema kati ya thamani ya uwekezaji huo, Dola za Marekani bilioni 9.60 zimetokana na uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (FDI), huku uwekezaji wa ndani ukichangia Dola bilioni 5.72, hali inayoonesha ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje katika kukuza uchumi.

Katika kuendelea kuvutia mitaji, TISEZA inaendeleza maeneo maalumu ya kiuchumi ya Bagamoyo, Kwala na Nala kwa ajili ya uwekezaji katika viwanda, uchakataji wa mazao, biashara na huduma za usafirishaji.

Teri amesema juhudi za kutangaza maeneo hayo zimewezesha kupokea maombi zaidi ya 80 ya matumizi ya ardhi, ambapo maombi 43 yamefikia hatua ya kusainiwa kwa mikataba ya upangishaji au haki za upangaji wa ardhi.

Ameeleza kuwa maombi hayo yanatarajiwa kuvutia uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.5 na kuzalisha ajira zaidi ya 15,844. Amesema hatua hiyo inadhihirisha umuhimu wa kuendeleza maeneo maalumu ya kiuchumi yenye miundombinu inayokidhi mahitaji ya wawekezaji.

Uendelezaji wa maeneo hayo unatarajiwa kuongeza kasi ya uwekezaji, kukuza uzalishaji wa bidhaa na huduma pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.