HOMERA ATAKA WATANZANIA WANUFAIKE ZAIDI NA SEKTA YA MAFUTA NA GESI

DAR ES SALAAM

Serikali imelitaka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuandaa mkakati maalumu wa kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia, ukiwa na muda wa kuwasilishwa kabla ya Desemba 31, 2026.

Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, ametoa agizo hilo leo, Novemba 16, 2026, wakati akifungua Kikao cha Sita cha Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi la PURA jijini Dar es Salaam.

Amesema ni muhimu kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli zote za mkondo wa juu wa petroli ili rasilimali hizo ziweze kutoa manufaa mapana kwa taifa. Amesisitiza kuwa mkakati huo uzingatie maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, wakati wa hafla ya kukabidhi leseni kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Dkt. Homera pia ameitaka PURA kuimarisha usimamizi wa shughuli za mafuta na gesi na kushirikiana na taasisi nyingine za sekta ya nishati katika kutekeleza ajenda ya mpito wa nishati. Amesema Tanzania inapaswa kutumia rasilimali zake za gesi asilia kwa maendeleo ya wananchi, sambamba na kuzingatia matumizi ya nishati safi na teknolojia za kukamata na kuhifadhi hewa ukaa (CCS).

Ameipongeza PURA kwa ushauri wa kitaalamu uliowezesha Serikali kutoa leseni nne za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa TPDC katika vitalu vya Lindi-Mtwara, Eyasi-Wembere, Songo Songo Magharibi na Mnazi Bay Kaskazini.

Aidha, amesema ushiriki wa mamlaka hiyo katika mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi katika Kitalu cha Mnazi Bay umechangia kugunduliwa kwa futi za ujazo bilioni 223 za gesi asilia katika kisima cha KASA-1X, pamoja na kuongeza uzalishaji katika visima vingine. Mradi huo pia umewezesha ajira kwa Watanzania takribani 350 na kutoa zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 20 kwa watoa huduma wa ndani.

Katika hatua nyingine, Homera amesema Wizara ya Nishati inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya mafunzo ya watumishi wa PURA na wizara hiyo ili kuongeza ujuzi na uwezo wao wa kitaalamu katika kutekeleza majukumu ya kusimamia sekta ya mafuta na gesi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.