TARURA YAONDOA KIKWAZO CHA MTO NATENE KWA DARAJA LA KISASA

Rukwa.

Wananchi wa Kata za Namanyele na Isunta wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, wameondokana na changamoto ya kuvuka Mto Natene wakati wa mvua baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 44 kwa gharama ya Sh milioni 192.

Daraja hilo lililojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) limekamilika kwa asilimia 100 na kuunganisha maeneo hayo ambayo kwa muda mrefu yalitenganishwa na mto, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za kijamii na huduma za kila siku, hasa wakati wa masika.

Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Nkasi, Mhandisi Madirisha Lumala, amesema awali wananchi walitegemea daraja la muda ambalo halikuwa salama, huku baadhi wakipoteza maisha wakijaribu kuvuka mto huo. Ameeleza kuwa hali hiyo ilifanya Serikali kuona umuhimu wa kujenga daraja la kudumu ili kuimarisha mawasiliano kati ya kata hizo.


Amesema daraja hilo pia litawanufaisha wanafunzi wanaosafiri kutoka Namanyele kwenda Shule ya Msingi Isunta na wanaotoka Isunta kwenda Shule ya Sekondari Mkangale iliyopo Namanyele, ambao awali walikumbwa na changamoto ya kukatika kwa mawasiliano wakati mto ulipojaa maji.

Mhandisi Lumala amesema daraja hilo limejengwa kwa kutumia teknolojia ya mawe, ambayo imepunguza gharama kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na matumizi ya zege na nondo. Ameeleza kuwa ujenzi kwa teknolojia hiyo umegharimu Sh milioni 192, wakati makadirio ya kutumia zege na nondo yalikuwa kati ya Sh bilioni 3.5 na bilioni nne.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyele, Crispin Wikula, ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza mradi huo, akisema utarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali na maeneo ya ibada.

Mkazi wa Mabatini mjini Namanyele, Christina Kalungizi, amesema daraja hilo limeondoa hofu ya kuvuka mto, hasa wakati wa dharura usiku, ambapo sasa wananchi wanaweza kutumia usafiri wa bodaboda kwa urahisi na gharama nafuu.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.