Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu na wasimamizi wa vituo vya hali ya hewa kutumia mifumo ya kisasa ya kimataifa ili kuongeza ubora na kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinakusanywa na kusambazwa kwa wakati.

Morogoro. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu na wasimamizi wa vituo vya hali ya hewa kutumia mifumo ya kisasa ya kimataifa ili kuongeza ubora na kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinakusanywa na kusambazwa kwa wakati.

Jitihada hizo zimejikita katika matumizi ya mifumo ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), ikiwemo Mfumo Jumuishi wa Kimataifa wa Uangazi wa Hali ya Hewa (WIGOS), kwa kuzingatia viwango vya Mtandao wa Kidunia wa Uangazi wa Hali ya Hewa (GBON).

Akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wataalamu hao iliyofanyika katika Hoteli ya Morena, Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema matumizi sahihi ya mifumo hiyo yatasaidia vituo kukusanya na kuwasilisha data zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Chang’a, ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa WMO na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa SOFF unaolenga kuboresha miundombinu ya uangazi na mifumo ya upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa.

Ameeleza kuwa Tanzania inajiandaa kutekeleza matakwa ya GBON kupitia vituo 27 vya uangazi wa hali ya hewa ardhini na vituo vitano vya uangazi katika anga za juu, huku lengo likiwa nchi kuwa tayari kutimiza matakwa hayo ifikapo Desemba 2027.

Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Miundombinu wa TMA na Mratibu wa Mradi wa SOFF, Dkt. Pascal Waniha, amesema warsha hiyo inalenga kuwajengea uwezo Mameneja wa Kanda, wasimamizi wa vituo na wataalamu kutumia mifumo ya OSCAR na WDQMS kutathmini uwezo wa vituo, kupima ubora wa data na kubaini changamoto ili zichukuliwe hatua kwa wakati.

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TMA kuhakikisha miundombinu ya hali ya hewa inafanya kazi kwa ufanisi na kuzalisha taarifa za kuaminika zitakazotumika nchini na katika mifumo ya kimataifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.