KINANA APOKEA WANACHAMA WAPYA WA CCM 1,167 KUTOKA SENETI YA VYUO VIKUU MBALIMBALI NCHINI.


DAR ES SALAAM.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka vijana kujitokeza wa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi huku kikiahidi kuwapa fursa kwa kuwapitisha kwa kuwa wanao uwezo wa kuongoza.

Akizungumza katika mkutano mkuu maalumu wa ukaribisho wa wananchama wapya 1,167 wa Seneti ya Vyuo Vikuu wa DIT, CBE, IFM na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kutoka tawi la Kibasila, Kata ya Upanga Mashariki Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana Amesema chama kinawategemea vijana kwa kuwa wanayo chachu ya mawazo ya kuendeleza chama, hivyo wasifikiri kuwa kuna sehemu nyingine mawazo yatatoka bali watambue kuwa wao ni taifa la leo.

Amesema Chama kinawategemea kwa ushauri, kujenga hoja na kukosoa, hivyo watambue wao ni watu wa kisasa, wasomi na wanakwenda na kasi ya upatikanaji wa taarifa hususan kupitia mitandao ya kijamii.

"Kutokana na hilo mnao uwezo mkubwa wa kutushauri, kutujenga na kutukosoa, tunakutegemeeni sana, toeni mawazo. mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa, nawasihi vijana jitokezeni na gombeeni katika nafasi zote," alisema.

Kinana ameongeza kuwa Chama kitafanya kila linalowezekena kuwapitisha vijana wengi katika nafasi za kugombea kwani yeye na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan watafanya kila jitihada kuwapitisha vijana wengi.

"Nawasihi nendeni mkagombee nafasi zote na Chama tutatoa maelekezo kufanya linalowezekena kuhakikisha vijana wanapewa nafasi nanyi hakikisheni mnakipa ushindi Chama chenu," alisema.


Ameongeza kuwa CCM ni kubwa, hivyo wanapaswa kukilinda, kujipanga, kuweka mikakati na kugawa majukumu.

Amebainisha kuwa yapo mambo yanayochangia kukipa ushindi Chama ukiwemo utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo aliwataka vijana kuchagua viongozi wenye uwezo na sio wa kubebwa wala kutumia fedha kupata nafasi.

Hata hivyo, alisema Chama kisingependa kupata malalamiko bali kitachagua viongozi kulingana na sifa zao.

Kinana ameahidi kutoa kompyuta, mashine ya kuchapisha na 'printa' kwa vijana hao wajitegemee katika seneti yao.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.