VIJIJI 70 VYA NUFAIKA NA FORVAC.



Na Mwandishi Wetu,

Dar es salaam .      

ZAIDI ya vijiji 69 vya mikoa ya Tanga, Mkangara, Dodoma, Lindi na Ruvuma vimenufaika kiuchumi, kijamii na mazingira kupitia Mradi wa Kuongeza Mnyororo wa Thamani kwenye Mazao ya Misitu (FORVAC).

Mradi huo ambao ulianza mwaka 2018 na kufikia mwisho mwaka Julai mwaka 2024 umewezesha vijiji 69 kupata zaidi ya Sh bilioni 9 kwa kipindi cha miaka sita, ambazo zimetumika kutekeleza miradi ya kijamii.      

Hayo yamesemwa na Mtaala wa Misitu kutoka Mradi wa FORVAC, Marcel Mutunda wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo amesema mradi huo umefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 100.      

Mutunda amesema mradi huo ambao umehusisha hekta 460,000 kati ya 450,000 ambazo zilipangwa awali umeweza kugusa jamii kubwa ya vijijini, huku uhifadhi kuboreka.

"Mradi wa FORVAC umehusisha mikoa mitatu ambayo ni Kongani ya Tanga iliyokuwa na Wilaya ya Handeni, Kilindi, Kiteto mkoani Manyara na Mpwapwa Dodoma, Kongani ya Ruvuma ilihusisha Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Songea, Namtumbo na Tunduru na Kongani ya Lindi ni Wilaya ya Nachingwea, Ruangwa na Liwale ambapo vijiji zaidi ya 69 vimegeswa na mradi," amesema.                       

Mtaalam huyo wa misitu amesema kupitia mradi huo hekta 460,000 zimehifadhiwa kwa mfumo wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) na kuwaingiza wanavijiji zaidi ya Sh bilioni 9 ambazo zimetumika kujenga shule, zahanati, visima vya maji, wananchi kukata bima ya afya na nyingine nyingi.                   

Amesema wananchi ambao wamenufaika na program hiyo wameweza kuongeza kipato na kuishi maisha bora, huku misitu ikiwa endelevu.            

Mutunda amesema pamoja na mafanikio ambayo wamepata wamekutana na changamoto ya mipaka ya vijiji hasa vile ambavyo havikuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.                        

"Pia moto holela ilichangia utekelezaji wa mradi kusuasua na mifugo kuingia kwenye msitu ni baadhi ya changamoto tulizokumbana nazo," amesema.                           

Mratibu wa FORVAC Taifa, Emma Nzunda amesema mradi huo umekuwa na matokeo chanya kwa wanavijiji na serikali kwa ujumla.             

Nzunda amesema mradi umewezesha wizara kutengeneza miongozo, kutafsiri sera na miongozo, kutafutia wanufaika masoko, hivyo wamenufaika kiuchumi

Aidha amesema mradi huo umewezesha wanavijiji kupata mashine za kisasa, kifaa cha kukausha mbao, hivyo bidhaa za misitu kwenda sokoni zikiwa na ubora na thamani kubwa.     

"FORVAC imeweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya misitu na uhifadhi, tunatarajia kuja na mradi mwingine ambao utaendeleza ilipoishia FORVAC," amesema.                               

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Misitu Wizara ya Maliasili na Utalii, Deusdedit Bwoyo amesema wiraza itahakikisha mazuri yaliyopatikana kupitia mradi huo yanaendelezwa kwani uhifadhi una faida kwa kimazingira, kijamii na kiuchumi            

Amesema Tanzania kuna hekta milioni 48.1 ya misitu ambapo hekta milioni 22 zipo kwenye ardhi za vijiji, hivyo kupitia mradi huo wameona umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi katika kuisimamia na kuitunza.     

"Mradi huu umegusa hekta 460,000, ila lengo letu kama wizara ni kufika Tanzania yote, hivyo naomba wadau wengine wa uhifadhi waje tushirikiane," amesema.                            

Amesema mradi huo ambao unaisha Julai mwaka huu unapaswa kuendelezwa na Watanzania wote kwa kuwa una faida kwa nchi. 

Naye Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Finland, anayeshughulikia Masuala ya Maliasili, Sanna Liisa Taivalmaa amesema nchi yao itaendelea kusaidia Tanzania kwenye eneo hilo kwani ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.         

Amewataka Watanzania kuthamini na kutambua faida ya misitu kwani ni muhimu kiuchumi, kijamii na mazingira.

Amesema iwapo wananchi watashirikishwa katika uhifadhi wa misitu ni wazi kuwa mafanikio yatakuwa mengi zaidi kuliko hasara.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.