Na Mwandishi Wetu,
Arusha
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) utatoa ajira kwa vijana wazawa 143 kutoka nchini Tanzania na Uganda waliofuzu mafunzo ya kozi maalum ya nishati za gesi na mafuta iliyoendeshwa kwa njia ya mtandao ‘Massive Open Online’ (MOOC) ili kupata ajira katika mradi huo unaoanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga
.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo mkoani Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP Bw. Guillaume Dulout alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo vijana wazawa kwa kuwapa maarifa yatakayotoa mchango stahiki katika kukuza sekta ya mafuta na gesi sambamba na kuwanufaisha wananchi wa Tanzania na Uganda wanaopitiwa na mradi huu.
Takriban vijana 2,000 walijiandikisha, huku 143 wakifaulu na kupata ajira katika awamu hii.
" Ili kuwapa vijana wazawa wa nchi hizi mbili (Tanzania na Uganda), ujuzi na maarifa kuhusu sekta ya gesi na mafuta, tumeamua kutoa mafunzo haya ili kutoa ujuzi na maarifa kwa jamii zinazopitiwa na mradi huu ili kuja kuwa na wataalamu watakaotumika katika miradi mingine pindi mradi huu utakapoisha." Alisema Bw. Dulout.
Kwa upande wake Meneja mafunzo kutoka EACOP, Bw. Laurent Stephane, alisema mafunzo hayo ni ishara ya wazi katika kuchochea maendeleo endelevu katika sekta ya mafuta na gesi baina ya nchi hizo mbili sambamba na kuwa na vijana wataalamu ambao ni wazawa.
“EACOP inaendelea kutilia mkazo maendeleo ya vipaji vya wazawa na imejipanga kukuza ukuaji wa uchumi na uendelevu katika ukanda huu,”
“Uzinduzi wa mafunzo haya ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba manufaa ya sekta ya mafuta na gesi yanashirikishwa kwa upana, hasa miongoni mwa vijana ambao ni nguzo ya mustakabali wa mataifa haya,” alisema Bw. Stephane.
Naye Mratibu wa mradi huu kwa upande wa Tanzania kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Bw. Asiadi Mruto alisema ujenzi wa mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 43.5% ambapo miundombinu ya ujenzi inaendelea kwa upande wa Tanzania na Uganda.
“Mafunzo haya yataanza kwa awamu tofauti awamu ya kwanza, wanafunzi watajifunza kwa miezi miwili katika chuo cha ufundi Arusha (ATC) na baadaye watapelekwa kwenye chuo cha Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) Moshi ambapo watajifunza kwa mda wa miezi mitatu baada ya hapo watapelekwa nchini Uganda kwenye chuo cha Uganda Petroleum Institute Kigumba (UPIC) ambapo pia watapata mafunzo kwa muda wa miezi sita na mwisho wataenda nchini Ufaransa kumalizia mafunzo yao ambayo yataangazia zaidi mradi wa EACOP,” alisema Bw. Mruto.
Katika hatua nyingine, Mruto amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu hassan imejidhatiti katika kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafikia malengo yaliyowekwa.
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kanda ya Kaskazini Bi. Monica Mbele alisema chuo cha Veta Moshi pia kitatumika kutoa mafunzo kwa vijana hao 143.
“Tumefaidika sana kwa ujio wa mradi huu kwani walimu wetu wameweza kupata mafunzo mbalimbali kutoka kwa wataalamu wabobezi kutoka makampuni za kimataifa,” alisema Bi. Mbele.
Alisema EACOP imeendelea kufanya maboresho katika chuo hicho, ambapo tayari wameshatoa fedha kwa ajiri ya ukarabati wa majengo ikiwemo mabweni na madarasa sambamba na vifaa vya kisasa vya kufundishia kulingana na fani zitakazotolewa hivyo mashirikiano hayo yamekuwa na tija si kwa wanafundi na walimu pekee bali kwa chuo kizima.
Bw. Oikitoki Lumenyo ambaye ni mnufaika wa mafunzo hayo alisema kupitia elimu anayopata itamsaidia kwenda kuwaelimisha jamii yake ya kimasai faida za mradi huo ikiwemo kufanya kazi kimataifa kwenye miradi mikubwa yakimkakati.
Wana hisa wa mradi wa EACOP ni Total Energies ikimiliki asilimia 62, Mashirika ya kusimamia mafuta nchini Tanzania (TPDC) na UNOC ya Uganda yakimiliki asilimia 15 kila moja, wakati shirika la mafuta nchini China (CNOOC) linamiliki asilimia nane tu.
Hakuna maoni: