RAIS SAMIA AZINDUA SOKO LA MADINI YA VITO NA DHAHABU TUNDURU.










Tunduru,Ruvuma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania *Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan* amezindua Soko la Madini ya Vito na Dhahabu Wilayani Tunduru ikiwa ni moja ya shughuli alizofanya akiwa katika ziara ya kikazi ya siku 6 Mkoani Ruvuma. 


"Kwa dhati kabisa, napenda kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa utekelezaji wa Sera ya kushirikiana na sekta binafsi yaani Public Private Partnership kwa vitendo ambapo Serikali imeweka fedha kiasi na kiasi kingine kimechangiwa na wafanyabiashara wa madini waliopo hapa Wilayani Tunduru"


"Ni dhahiri kwamba ujenzi wa soko hili kubwa na la kisasa utarahisisha biashara ya madini Wilayani hapa na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji maduhuli ya Serikali sambamba na kudhibiti udanganyifu na utoroshaji wa madini", alibainisha Mhe. Rais.


Aidha, Rais Samia ameonesha wazi kufurahishwa na ushirikiano huo wa Halmashauri na Sekta binafsi na kusisitiza kwamba Sera ya PPP ikitelezwa kwa vitendo ni chachu ya maendeleo ya wananchi katika Wilaya zote nchini.


Pia, Rais Samia alipongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika Mkoa wa Ruvuma ambapo alieleza kwamba kwa kipindi cha Mwezi Julai na Agosti, 2024 zaidi ya shilingi bilioni 6.5 zimekusanywa, hali inayoleta taswira nzuri ya makusanyo kadri muda unavyoendelea.


Katika hatua nyingine, Mhe. Rais alisisitiza na kutambua mchango wa wachimbaji wadogo katika uchumi wa Taifa, na kumwelekeza Waziri wa Madini kuhakikisha STAMICO inawasimamia ipasavyo na kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili wanufaike na rasilimali hiyo na kuongeza mchango wao kwenye pato la Taifa kwa ujumla.


Awali, akitoa maelezo mafupi ya sekta ya madini, Waziri wa Madini *Mhe. Anthony Mavunde* alibainisha kuwa ikiwa ni matokeo ya Sera nzuri na mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, mwaka wa fedha uliopita sekta ya madini ilikusanya na kuchangia kwenye mfuko mkuu wa Serikali Shilingi bilioni 753 ilhali kwa mwaka 2015/2016 ni shilingi bilioni 161 pekee zilikusanywa.


"Maelekezo yako Mhe. Rais ndiyo yamepelekea kwa mwaka 2023/2024 zaidi ya shilingi trilioni 1.7 zizunguke kwenye masoko 43 na vituo vya ununuzi 102 nchi nzima kwenye biashara ya madini. Pamoja na mzunguko huo, sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi na kuchangia ukuaji wa vipato vya wananchi katika maeneo mbalimbali" alisema Mhe. Mavunde. 


"Katika kipindi cha siku 84 za mwaka huu wa fedha yaani 2024/2025 tayari sekta ya madini imekusanya jumla ya shilingi bilioni 225 na kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali, hii ni hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya madini na ukuaji wa uchumi wa Taifa letu" aliongeza Mhe. Mavunde.


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, *Mhe. Hassan Zidadi Kungu* ameipongeza Serikali kwa miradi ya maendeleo inayofanyika katika eneo lake na kutia shime suala la Serikali kuendelea kuwaunga mkono wachimbaji wadogo. Aidha, aliiomba Serikali kuangalia katika mipango ya baadae ujenzi wa soko kubwa la ghorofa la madini ili kutoa nafasi kwa wanunuzi wengi ambao wanaongezeka siku hadi siku.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.