TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MASUALA YA NISHATI BARANI AFRIKA UTAKAOUCHAGIZA KUKUSANYA DOLA ZA MAREKANI BILIONI 190.
Fedha hizo zinalengwa kufikisha umeme kwa wananchi milioni 300 barani humo ifikapo mwaka 2030.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye mkutano wa kujadili ajenda ya upatikanaji wa nishati Afrika amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika mwakani, 2025
“Wameridhishwa na utendaji kwenye sekta ya nishati, wameridhishwa na mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme mpaka vijijini, siyo tu vijijini lakini mpaka kwenye kila nyumba. Wameamua kuitisha mkutano mkubwa barani Afrika ambao utawakutanisha wadau mbalimbali, taasisi za Kimataifa na taasisi zinazotoa mikopo kwa wajasiriamali na makampuni ili waweze kuwekeza kwenye umeme.” alisema Mhe. Majaliwa katika hotuba yake
Mkutano huo ulioandaliwa na taasisi ya Global Energy Alliance for People and Planet (GEAPP) jijini New York, Marekani, umeruhusu kujadiliwa kwa mambo ya msingi juu ya Nishati safi na endelevu kwa bara zima la afrika.
Akifafanua kwa undani, Mhe. Majaliwa Alisema kuwa mkutano huo ambao utaendeshwa kwa pamoja baina ya Benki ya Dunia, Benki ya ADB na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, unatarajiwa kuwaunganisha viongozi, waatalamu wa viwandani na asasi za kiraia ili kuwezesha upatikanaji wa nishati za uhakika, teknolojia bora za nishati safi na sera endelevu.
“Ninaipongeza Serikali ya Norway na taasisi ya Rockefeller kwa kuamua kuunga mkono jitihada za Benki ya Dunia na ADB za kuhakikisha umeme unapatikana kwa watu milioni 300 ifikapo mwaka 2030. Mpango huu ni wa muhimu hasa kwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako watu zaidi ya milioni 600 hawana fursa ya kupata umeme. Hatuwezi kuwa na maendeleo endelevu kama hatutashughulikia kwa haraka changamoto hii,” alisema.
Katika hotuba yake, Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina alisema wanawake milioni 900 wanataabika kwa kukosa nishati safi ya kupikia na kila mwaka ilhali upishi unapaswa uwe ni wa staha.
“Wanawake milioni 130 wanatakiwa wawe wamefikiwa na huduma hii kila mwaka. Tunapoteza wanawake na watoto wengi kwa sababu ya kukosa huduma hii.” aliongezea Dkt. Adesina.
Wakati huohuo, Rais wa Liberia, Joseph Boakai, alisema kuwa umeme ni muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na unapaswa kupewa kipaumbele zaidi kwani bila umeme hakuna maendeleo
“Nchini Liberia, maeneo mengi ya vijijini yako gizani, na maeneo yenye umeme hayafikii asilimia 20. Unawezaje kupanga ajenda za maendeleo kama hauna umeme? Unawezaje kwenda hospitali wakati hakuna umeme? Hili ni suala nyeti na hatupaswi kuendelea kulisubiria kwa muda mrefu,” alisisitiza.
Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kitaifa, Balozi Thabit Kombo, Waziri wa Nchi (OR-Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Afya wa SMZ, Nassor Ahmed Mazrui na watendaji wengine wa Serikali.
Hakuna maoni: