BABA HARUSI ANASWA: POLISI WAMFICHUA KWA UDANGANYIFU WA GARI NA MAMILIONI; ALIJITEKA NA KUJIFICHA KWA MGANGA.


DAR ES SALAAM.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam tarehe 15 Desemba, 2024 lilimpata na kumshiklia Vicent Peter Massawe maarufu kama baba harusi Mkazi wa Kigamboni Dar es salaam kwa tuhuma za Kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu (CDS/IR/2065/2024) na wizi wa kuaminiwa (CDS/IR/2066/2024), baada ya kutengeneza mazingira ya uongo ya kupotea na kutenengeza hisia kwa umma kuwa ametekwa na baadae kwenda kujificha Pemba Chakechake Mgogoni kwa mganga wa kienyeji aitwaye Hamis khalid.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam Muliro J. Muliro -SACP amesema Ufutiliaji na mahojiano ya kina kati ya Polisi na mtuhumiwa (baba harusi) baada ya kupatikana alikiri kutenda makosa hayo ambapo alichua pesa kwa udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali ikiwa ni pamoja TZS mililioni 55 na gari namba T 642 EGU aina Toyota Ractis kwa udanganyifu kutoka kwa bwana Sylivester Beda Massawe. Alichukua tena pesa Tshs mil. 10 kwa udanganyifu kutoka kwa Ramadhani mkazi wa Magomeni, Alichukua pesa pia kwa udanganyifu milioni.15 kutoka kwa Ramadhani Bakari mkazi wa Temeke. 


"Mtuhumiwa alichukua pesa pia kwa udanganyifu mil.5 kutoka kwa Resma Mbuguni HR CBE. Alichukua pesa tena mil.4 kutoka kwa Asia Mohamed mkazi Madale. Kwa udanganyifu alichukua tena mil.1.5 kutoka kwa Ngoma mkazi wa Kibaha. Aliendelea tena kwa udanganyifu kuchukua mil.8 kutoka kwa Fauz Suleimani Mussa mkazi wa Tabata baada ya kumuuzia gari ambalo sio lake aliloliazima siku ya harusi yake. Gari namba T642 EGU Ractis mali ya Sylivester Beda Massawe".

Ikumbukwe kuwa tarehe 19 Novemba, 2024 Polisi Kigamboni ilipokea taarifa ya kupotea kwa Vicent Peter Massawe Mfanyabiashara ambaye ilidaiwa hakuonekana toka tarehe 18 Novemba, 2024 baada ya harusi yake na alipotea huku akitumia gari Toyota Ractis no T 642 EGU ya Sylvester Masawe ambayo baadae ilibainika mtuhumiwa aliiuza badala ya kuirudisha kwa mwenyewe baada ya harusi yake tarehe 16 Novemba 2024 kwenye ukumbi wa Golden Jubilee.

Uchunguzi wa mashauri haya unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa katika mamlaka nyingine za kisheria kwa hatua zaidi.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuwa watulivu pindi wapatapo taarifa kuhusiana na matukio ya namna hii na kuviacha vyombo vya kiuchunguzi kufanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka zingine na wananchi. 

Aidha Jeshi la Polisi linawaonya na kuwatahadharisha kikundi cha watu wanne ambao kazi yao ni kujenga taharuki kwa umma kuwa kila anayepotea au kutoonekana wao hujitokeza na kuandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa watu hao wamechukuliwa na gari hard top nyeupe na kulazimisha hisia kuwa ni vyombo vya dola vimehusika. 

"Melengo makubwa ya kundi hilo ni kutoa taarifa za uzushi zenye taharuki kwa lengo la kuichonganisha Serikali, Polisi na Wananchi. Jeshi halitasita kuwachukulia hatua kali na za kisheria wahusika ili kukomesha tabia hizo".

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea kuwashukuru wananchi ambao wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za kweli ambazo zimesadia kufanikisha masuala ya kiuchunguzi



Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.