Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) – Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imewataka wauzaji wa mbegu za mbogamboga kuhakikisha wanauza mbegu zenye ubora na zenye lebo halali kutoka TOSCI.
Akizungumza na vyombo vya habari, Bw. Meshack Mhesi kutoka TOSCI amesema taasisi hiyo inaendelea na ukaguzi wa maduka ya mbegu katika mikoa yote ya kanda hiyo kwa muda wa wiki tatu, ili kubaini kama wauzaji wanazingatia vigezo vya kisheria.
Amesema baadhi ya maduka yamekutwa yakiuza mbegu zisizokidhi viwango vya ubora, zikiwemo mbegu zisizo na lebo ya TOSCI, na hivyo wamezifungia mbegu hizo hadi makampuni yanayozalisha yaziwekewe lebo rasmi kutoka TOSCI. Hatua hiyo inalenga kulinda wakulima dhidi ya hasara ya kununua mbegu hafifu.
Kuhusu mbegu zinazouzwa kupitia mfumo wa ruzuku, Bw. Mhesi amesema wamebaini kuwa wakulima wengi wanazingatia masharti na kuuza mbegu za mahindi kupitia mfumo huo ipasavyo.
Amewashauri wakulima kuhakikisha wananunua mbegu zilizoidhinishwa na TOSCI pekee ili kuepuka kupata mazao duni kutokana na kutumia mbegu zisizo na ubora.
Kwa upande wao, baadhi ya wauzaji wa mbegu mkoani Njombe akiwemo Bi. Agape John Luoga, wameahidi kufuata maelekezo ya TOSCI, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na makampuni ya mbegu ili kuhakikisha wanapata mbegu zilizo na lebo halali ya TOSCI.
Hakuna maoni: