Na Mwandishi Wetu.
Serikali imethibitisha kuwa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Mzizima Towers unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) jijini Dar es Salaam umefikia hatua ya juu ya utekelezaji, ukiwa umekamilika kwa asilimia 91, huku ukitarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, Desemba 31, 2026.
Taarifa hiyo ilitolewa Machi 16, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipokuwa akiwasilisha maendeleo ya mradi huo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.Kwa mujibu wa maelezo yake, mradi huo mkubwa unahusisha ujenzi wa majengo mawili ya kisasa; jengo la biashara lenye ghorofa 35 pamoja na jengo la makazi lenye ghorofa 32. Kwa pamoja, majengo hayo yanachukua eneo la zaidi ya mita za mraba 95,000.
Amesisitiza kuwa usanifu wa majengo hayo umezingatia viwango vya kimataifa ili kukidhi mahitaji ya kisasa katika sekta za biashara, makazi na utalii, hasa katika jiji la Dar es Salaam linaloendelea kukua kwa kasi.
Aidha, mradi huo utakapokamilika utakuwa na hoteli ya kifahari ya nyota tano itakayoendeshwa na Radisson Hotel Group, ikiwa na vyumba 156 vya wageni pamoja na vyumba 132 vya makazi ya muda mfupi (hotel apartments).
Waziri Sangu alieleza kuwa NSSF inatekeleza mradi huo kwa asilimia 100 kama sehemu ya mkakati wake wa kuwekeza kwenye miradi mikubwa yenye faida kwa wanachama na taifa kwa ujumla. Aliongeza kuwa uwekezaji huo utasaidia kuongeza thamani ya mali za Mfuko pamoja na kuimarisha uwezo wake wa kutoa mafao.
Baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Hawa Mchafu Chakoma, alieleza kuridhishwa na maendeleo ya kazi na kupongeza juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha mradi unaendelea.
Amesema kamati imejionea ubora wa kazi inayofanyika na kuipongeza NSSF pamoja na uongozi wake kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Wajumbe mbalimbali wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao Hawa mchafu chakoma, akiwemo waipongeza NSSF kwa uwekezaji huo mkubwa, wakieleza kuwa utakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.Inatarajiwa kuwa mradi wa Mzizima Towers utakapokamilika utaleta manufaa mbalimbali ikiwemo kuongeza mapato ya Serikali na Mfuko, kukuza biashara na utalii, pamoja na kuongeza ajira. Zaidi ya watu 300 tayari wamepata ajira wakati wa ujenzi, huku ajira zaidi ya 250 zikitarajiwa kupatikana mara baada ya kuanza kwa shughuli ndani ya majengo hayo.








Hakuna maoni: