DAR CITY WAPATA MWALIKO BUNGENI, DIDI​ER DROGBA AWAPA HAMASA KUELEKEA BAL FINALS

DODOMA. 

Timu ya Dar City jana ilipata heshima ya kipekee baada ya kualikwa Bunge la Tanzania kushiriki katika usikilizaji wa bajeti ya Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, kwa mwaka wa fedha 2026/2027, tukio lililowapa fursa ya kujionea kwa karibu mchakato wa maamuzi ya kisera katika sekta ya michezo.

Mbali na hilo, wawakilishi wa timu hiyo walipata nafasi adhimu ya kukutana na kuzungumza na gwiji wa soka barani Afrika, Didier Drogba, ambaye aliwapa maneno ya hamasa na kuwataka kujiamini pamoja na kucheza kwa nidhamu wanapoelekea kwenye michuano mikubwa.

Akizungumza na wachezaji hao, Drogba aliwasisitiza umuhimu wa mshikamano na juhudi binafsi ili kufikia mafanikio makubwa katika mchezo huo.

Dar City sasa inaelekeza nguvu zake katika kujiandaa na fainali za Basketball Africa League zitakazofanyika jijini Kigali mwishoni mwa mwezi huu, ambapo wanatarajia kufanya vizuri na kuiwakilisha Tanzania kwa heshima.

Ushiriki wao katika jukwaa la kitaifa na kukutana na nyota mkubwa kama Drogba umeonekana kuwa chachu mpya ya morali kwa kikosi hicho, kinacholenga kuandika historia katika mashindano hayo ya kimataifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.