Licha ya kuripotiwa kushuka kwa zaidi ya asilimia 22 katika soko la dunia, watumiaji wa Afrika, Asia na Ulaya wanaweza kuendelea kununua mafuta kwa bei za zamani kwa miezi kadhaa ijayo.
Na. Mwandishi wetu,
Wakati bei ya mafuta ghafi duniani ikiripotiwa kushuka kwa zaidi ya asilimia 22 baada ya kupungua kwa hofu ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, wataalamu wa nishati wanaeleza kuwa kushuka huko hakumaanishi moja kwa moja kuwa watumiaji wa mwisho wataanza kuona nafuu ya haraka kwenye vituo vya mafuta.
Taarifa zinaonyesha kuwa bado kuna sababu kadhaa zinazofanya soko la mafuta kuendelea kuwa katika hali ya kusubiri licha ya mwelekeo wa sasa kuonyesha dalili za utulivu.
Matamko ya kisiasa yanatikisa bei
Katika wiki za hivi karibuni, bei za mafuta duniani zimekuwa zikipanda na kushuka kutokana na matamko ya viongozi wa Iran, Israel na Marekani.
Taarifa za mashambulizi, vitisho vya kufungwa kwa Mlango wa Hormuz au kauli za kujibu mashambulizi zimekuwa zikisababisha bei kupanda ndani ya muda mfupi, huku taarifa za mazungumzo ya amani zikisababisha bei kushuka.
Kwa nchi nyingi za Afrika, Asia na Ulaya zinazotegemea mafuta kutoka soko la kimataifa, hali hii ina maana kuwa tukio moja la kisiasa linaweza kubadilisha mwelekeo wa bei wakati wowote.
Usalama wa Hormuz ni swali kubwa
Ingawa usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz umetajwa kuanza kuendelea, bado hakuna uhakika wa muda mrefu kuhusu usalama wa eneo hilo.
Inafahamika kuws takribani robo ya mafuta yanayosafirishwa duniani hupita katika njia hiyo muhimu ya biashara.
Ndiyo maana wawekezaji, wafanyabiashara wa mafuta na masoko ya fedha bado wanaendelea kuwa waangalifu.
Hofu yoyote mpya kuhusu Hormuz inaweza kusababisha bei kupanda tena hata kabla ya mafuta kupungua sokoni.
Bima za meli bado hazijashuka kikamilifu
Moja ya athari kubwa za mgogoro wa Mashariki ya Kati ilikuwa kupanda kwa gharama za bima kwa meli zinazobeba mafuta.
Licha ya hali kuanza kutulia, kampuni nyingi za usafirishaji bado zinakabiliwa na gharama kubwa za bima kutokana na tathmini za hatari zilizowekwa wakati wa mgogoro.
Hii ina maana kuwa mafuta yanaweza kununuliwa kwa bei ya chini, lakini gharama za kuyafikisha kwa watumiaji zikabaki juu.
Wafanyabiashara Bado wanauza Mafuta waliyonunuliwa kwa Bei ya juu Sababu nyingine muhimu ni kwamba mafuta mengi yanayotumika sasa katika masoko mbalimbali duniani yaliagizwa wakati bei za mafuta zilikuwa juu zaidi.
Kwa mfano, Tanzania na nchi nyingine nyingi za Afrika Mashariki huagiza mafuta wiki kadhaa au miezi kabla ya kufika kwa watumiaji.
Hivyo mafuta yanayouzwa leo yanaweza kuwa yalinunuliwa wakati bei ya pipa ilikuwa zaidi ya dola 100, tofauti na viwango vya sasa vilivyoshuka.
Kwa sababu hiyo, kushuka kwa bei ya mafuta ghafi duniani huchukua muda kabla ya kuonekana kwa watumiaji wa mwisho.
Tanzania Inaweza Kuanza Kuona Nafuu Mwezi wa Nane ikiwa hali ya kushuka kwa bei ya mafuta itaendelea katika soko la Dunia,
kwa upande wa Tanzania, wataalamu wa soko la nishati wanaamini kuwa kama bei za mafuta duniani zitaendelea kubaki katika viwango vya sasa na hakutatokea mgogoro mpya Mashariki ya Kati, athari za kushuka kwa bei zinaweza kuanza kuonekana taratibu kuanzia mwezi Agosti na kuendelea.
Hii itategemea kasi ya kuingia kwa mafuta mapya yaliyonunuliwa kwa bei za chini na kuondoka kwa akiba zilizopatikana wakati wa bei za juu.
Ni Mapema Kutabiri Nafuu ya Kudumu Pamoja na matumaini yaliyopo, soko la mafuta bado halijapata utulivu wa kudumu.
Tukio lolote jipya la kijeshi, tishio dhidi ya usafirishaji wa mafuta au matamko makali kutoka kwa viongozi wa mataifa yanayohusika na mgogoro linaweza kubadilisha hali ya sasa na kusababisha bei kuanza kupanda tena.
Hii ni kusema kuwa licha ya bei ya mafuta ghafi kushuka kwa zaidi ya asilimia 22 katika soko la dunia, watumiaji wa Afrika, Asia na Ulaya bado wanaweza kuendelea kununua mafuta kwa bei zinazokaribiana na zile za kipindi cha mgogoro.
Sababu kubwa ni kuendelea kwa tahadhari za kiusalama, gharama za bima, athari za matamko ya kisiasa na ukweli kwamba sehemu kubwa ya mafuta yanayotumika sasa ilinunuliwa wakati bei zilikuwa juu.
Kwa sasa dunia inaendelea kuishi katika hali ya "panda shuka" ya bei za mafuta, huku nafuu halisi ikisubiri utulivu wa kudumu wa soko la nishati duniani.

Hakuna maoni: