Na Mwandishi Wetu,
PWANI-BAGAMOYO.
Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Hifadhi ya Magofu ya Kaole, Mei 1, 2026, imefanikisha tamasha la utalii lijulikanalo kama “Kaole Ruins Camping” lililovutia zaidi ya washiriki 80 kutoka Bagamoyo na maeneo mengine ya nje ya mji huo.
Tamasha hilo lililofanyika ndani ya Hifadhi ya Magofu ya Kaole na Afisa Utalii, lililenga kuhamasisha utalii wa kihistoria na asilia pamoja na kuitangaza urithi wa kipekee uliopo katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa tamasha hilo, Mhifadhi wa Maikale Kaole, Veronica Kombe alisema washiriki walipata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya kihistoria vilivyopo katika magofu hayo, ikiwemo misikiti ya kale, kisima cha maajabu, mbuyu wa maajabu, kaburi la wapendanao na eneo la bandari ya kale, pamoja na utalii wa mikoko.
Alieleza kuwa historia ya Magofu ya Kaole inarejea hadi karne ya 13, ambapo wageni wa awali walioweka makazi yao katika eneo hilo waliacha masalia ambayo leo yamekuwa kivutio kikubwa cha watalii wa ndani na nje ya nchi.
Baada ya ziara ya kihistoria, washiriki walipata burudani mbalimbali zikiwemo ngoma za asili za utamaduni wa Wazaramo, karaoke pamoja na michezo ya jadi kama bao, hali iliyoongeza mvuto wa tamasha hilo.
kwa upande wake, Mhifadhi wa Malikale, Winfrida Msaki alieleza kuwa washiriki wote walishiriki kwa kulipia tozo stahiki za Serikali, hatua inayochangia mapato na kuunga mkono juhudi za uhifadhi na maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
TFS imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuendeleza matukio ya aina hii ili kukuza utalii wa ndani na kuhamasisha jamii kutambua na kuthamini rasilimali za kihistoria na asilia zilizopo nchini.










Hakuna maoni: