DAR ES SALAAM.
Wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya taasisi za umma umetolewa ili kudhibiti na kupunguza athari za majanga ya moto, hasa katika maeneo ya mijini yenye shughuli nyingi za kiuchumi.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Zimamoto yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Wakili Albert Msando, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ametoa maagizo kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kushirikiana kwa karibu na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA).
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha miundombinu ya barabara na huduma za umeme inajengwa kwa kuzingatia viwango vya usalama, ili kurahisisha udhibiti wa majanga ya moto pindi yanapotokea.
Aidha, Msando amesisitiza umuhimu wa ukaguzi wa vifaa vinavyotumika kuunganisha umeme katika maeneo ya biashara, masoko na maduka, akibainisha kuwa wahusika watakaobainika kutumia vifaa visivyo salama wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania na Msemaji wa Jeshi hilo, DCP Puyo Nzalayaimisi, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulipatia jeshi hilo vifaa vya kisasa pamoja na magari ya uokoaji.
Amesema juhudi hizo zimeongeza uwezo wa jeshi hilo katika kukabiliana na majanga, huku akiahidi kuwa wataendelea kuwahudumia wananchi kwa kujituma na kwa weledi mkubwa.


Hakuna maoni: