NEMC YAADHIMISHA MIAKA 40 KWA KISHINDO, YAZINDUA MFUMO WA KIDIJITALI WA UFUATILIAJI UCHAFUZI WA MAZINGIRA



Na Mwandishi Wetu, 
Dar es Salaam. 

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameisisitiza jamii kupewa elimu endelevu kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira ili kuondoa tabia ya uharibifu wa mazingira inayochangiwa na ukosefu wa uelewa kwa baadhi ya wananchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kidijitali wa Ufuatiliaji na Uchambuzi wa Hali ya Uchafuzi wa Mazingira nchini (TOCEMS) pamoja na maadhimisho ya miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Nchemba aliliagiza baraza hilo kuendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya familia hadi jamii nzima.

Alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuimarisha usimamizi wa mazingira na kuhakikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo yanazingatia uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Masauni alisema Serikali inapanga kufanya maboresho mbalimbali ndani ya NEMC, ikiwemo kufanya mabadiliko ya kisheria yatakayowezesha taasisi hiyo kuwa mamlaka kamili yenye uwezo wa kujitegemea kifedha.

Akitoa maelezo kuhusu mfumo wa TOCEMS, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware alisema mfumo huo utawezesha kupatikana kwa taarifa za haraka kuhusu uchafuzi wa mazingira pamoja na uchambuzi wa viwango vya uchafuzi wa hewa, maji na kelele.

Alibainisha kuwa zaidi ya viwanda 100 tayari vimeunganishwa katika mfumo huo kwa ajili ya kurahisisha ufuatiliaji wa mazingira nchini.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Elizabeth Mrema alisema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Afrika kupata kiwango kikubwa cha ufadhili wa zaidi ya dola milioni 54 za Marekani kwa ajili ya miradi ya mazingira.

Aidha, alisema UNEP itaendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mazingira inayoweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, huku mfumo wa TOCEMS ukiwa tayari unatumiwa pia katika baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Nigeria na Ghana.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.