Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Ziara ya Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) katika mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) unaoendeshwa na kampuni ya Mofat katika eneo la Mbagala na kubaini mafanikio na changamoto kadhaa katika mradi huo muhimu wa usafiri jijini.
Katika mradi huo, mabasi hayo yanatarajiwa kutoa huduma ya usafiri wa haraka kwa wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani, ikiwa ni pamoja na kubeba abiria wa kawaida pamoja na huduma maalum kwa makundi kama wanafunzi na wafanyabiashara wadogo, hususan wa samaki, ili kurahisisha shughuli zao za kila siku.
Hata hivyo, zaidi ya mabasi 150 yaliyokusudiwa kuanza kazi katika mradi huo yameendelea kuegeshwa kwa zaidi ya nusu mwaka sasa bila kuanza kutoa huduma, licha ya kukamilika kwa maandalizi muhimu ikiwemo bima na taratibu nyingine. Changamoto kubwa inayotajwa ni ukosefu wa nafasi ya kuyaingiza katika baadhi ya maeneo ya uendeshaji, hali inayosababisha mabasi hayo kubaki katika kituo kikuu cha Rangi Tatu bila kutumika.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, alieleza kuwa kwa sasa ni mabasi takribani 50 pekee yanayofanya kazi, huku akibainisha kuwa hali hiyo inaleta hasara kwa mwekezaji kutokana na uwekezaji unaohusisha mikopo ya benki bila kurejesha mapato stahiki.
Kutokana na changamoto hiyo, DART kwa kushirikiana na mwekezaji wamekubaliana kuandaa ripoti ya tathmini ya nusu mwaka itakayowasilishwa serikalini kupitia Kamati ya Uendeshaji ya Ubia, kwa lengo la kutafuta suluhu ya kudumu na kuboresha utoaji wa huduma za usafiri jijini.



Hakuna maoni: