PUGU KAZIMZUMBWI: HAZINA YA UTALII INAYOHIFADHI HISTORIA NA BIOANUAI

Na Mwandishi Wetu, 

Pwani.

Hifadhi ya Msitu wa Asili ya Pugu Kazimzumbwi mkoani Pwani imeendelea kujidhihirisha kuwa moja ya hazina kubwa za utalii wa ikolojia nchini baada ya kuvutia wahifadhi kutoka Shamba la Miti Sao Hill waliotembelea eneo hilo kujifunza mbinu za uhifadhi, usimamizi wa bioanuai na maendeleo ya utalii endelevu.

Ziara hiyo imekuja wakati Tanzania ikiendelea kuimarisha juhudi za kuhifadhi rasilimali za misitu na kuendeleza utalii wa asili kama sehemu ya kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa, huku Pugu Kazimzumbwi ikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa kuhifadhi urithi wa kihistoria na mazingira ya kipekee karibu na Jiji la Dar es Salaam.

Wakati wa ziara hiyo, wahifadhi hao walitembelea vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo misitu ya asili yenye bioanuai adimu, njia za utalii wa kutembea msituni, maeneo ya kihistoria pamoja na vivutio vya kiikolojia vinavyovutia watalii wa ndani na nje ya nchi.

Maofisa wa hifadhi hiyo waliwaeleza wageni hao kuhusu hatua zinazochukuliwa kulinda mazingira, kudhibiti shughuli zinazohatarisha misitu na kuendeleza utalii wa ikolojia unaochochea maendeleo ya jamii na kuongeza mapato ya taifa bila kuathiri mfumo wa ikolojia.

Akizungumza baada ya kutembelea vivutio hivyo, Kiongozi wa Msafara huo, CO I Donald Makupa, alisema uzoefu walioupata katika Hifadhi ya Msitu wa Asili ya Pugu Kazimzumbwi utakuwa chachu ya kuboresha mikakati ya uhifadhi katika maeneo wanayoyasimamia.

“Tumeshuhudia namna ambavyo uhifadhi wa misitu unaweza kwenda sambamba na maendeleo ya utalii. Maarifa haya yatatusaidia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na kuongeza thamani ya maeneo yetu ya uhifadhi,” alisema Makupa.

Aliongeza kuwa ushirikiano na kubadilishana uzoefu kati ya taasisi na maeneo mbalimbali ya uhifadhi ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha sekta ya misitu na utalii inaendelea kukua kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wake, Afisa Utalii wa Hifadhi ya Msitu wa Asili ya Pugu Kazimzumbwi, Mbaruku Sinon, alisema ujio wa wahifadhi hao unaonesha namna maeneo ya uhifadhi yanavyozidi kuwa vituo vya kujifunzia na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za kulinda mazingira na kuendeleza utalii.

Alisema kuimarika kwa ushirikiano kati ya wahifadhi kutoka maeneo mbalimbali kutasaidia kuongeza ubunifu katika usimamizi wa rasilimali za misitu, kukuza idadi ya watalii na kuhakikisha bioanuai inayopatikana nchini inalindwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

“Pugu Kazimzumbwi ni zaidi ya hifadhi ya misitu. Ni darasa la uhifadhi, kituo cha utalii wa ikolojia na sehemu inayobeba historia muhimu ya nchi yetu. Tunahitaji kuendelea kushirikiana ili kuitangaza zaidi ndani na nje ya Tanzania,” alisema Sinon.

Katika ziara hiyo, wahifadhi hao walikumbushwa umuhimu wa kushiriki kampeni ya kuhamasisha wananchi kupigia kura vivutio vya utalii vinavyosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), hususan Pugu Kazimzumbwi Nature Forest Reserve na Amani Nature Forest Reserve, ambavyo vimeingia katika kinyang’anyiro cha Tuzo za Kimataifa za Utalii.

Wadau wa uhifadhi wanaamini kuwa mafanikio ya maeneo hayo katika tuzo hizo yataongeza mwonekano wa Tanzania katika soko la utalii duniani, kuvutia wageni wengi zaidi na kuchochea uwekezaji katika utalii wa asili unaozingatia uhifadhi wa mazingira.

Kwa miaka ya karibuni, Pugu Kazimzumbwi imeendelea kuwa kivutio muhimu kwa watalii, wanafunzi, watafiti na wadau wa mazingira kutokana na utajiri wake wa bioanuai, historia ya kipekee na ukaribu wake na Jiji la Dar es Salaam, hali inayoiweka katika nafasi ya kuwa moja ya nguzo muhimu za utalii wa ikolojia nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.