SALOME: NGUZO ZA ZEGE NA CHUMA KUTUMIKA KUKABILI CHANGAMOTO YA KUANGUKA KWA NGUZO ZA UMEME ZA MITI

DODOMA.

NAIBU Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema Serikali kupitia TANESCO inaendelea kubadilisha nguzo chakavu kwa kuweka nguzo imara zaidi, zikiwemo nguzo za zege na chuma, pamoja na kuimarisha misingi ya nguzo katika maeneo yenye udongo laini ili kukabili changamoto ya kuanguka kwa nguzo za umeme.

Salome ameeleza hayo leo, Mei 22, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Sara Msafiri Ally, Mbunge wa Mvomero, aliyetaka kujua ni lini Serikali itatatua changamoto ya kuanguka kwa nguzo za umeme katika Tarafa ya Mgeta.

Akijibu swali hilo, Salome amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya kuanguka kwa nguzo za umeme katika baadhi ya maeneo ya Tarafa ya Mgeta kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mvua nyingi, uwepo wa udongo usiohimilivu pamoja na uchakavu wa baadhi ya nguzo.

Amesema Serikali kupitia TANESCO inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya umeme ili kubaini na kushughulikia changamoto hizo mapema pindi zinapojitokeza.

Aidha, Salome amefafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imetenga bajeti maalum ya kubadilisha nguzo za miti katika maeneo yote yenye unyevunyevu pamoja na maeneo yenye shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Kadhalika, ametoa wito kwa wananchi kuacha matumizi mabaya ya ardhi, ikiwemo kuchoma moto ovyo mashambani, jambo ambalo limekuwa likiathiri miundombinu ya umeme kwa kuunguza nguzo za umeme.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.