Na Mwandishi Wetu,
Pwani.
UONGOZI wa Shule ya Awali na Msingi ya Courage iliyopo Kibamba wilayani Mkuranga, umetoa msaada wa chakula, mavazi na bidhaa mbalimbali kwa Kituo cha Watoto Yatima cha Lord’s Children Home kilichopo Kimanzichana wilayani humo.
Msaada huo ulikabidhiwa na Meneja wa shule hiyo, Theodosia Tarimo, ambaye alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utaratibu wa shule kusaidia jamii, hususan makundi yenye mahitaji maalumu.
“Uongozi, wafanyakazi na wanafunzi wa shule tumefika hapa leo kuwaletea furaha watoto hawa yatima na wenye mahitaji maalumu,” alisema Theodosia.
Alisema shule imeamua kufika kituoni hapo ili kusaidia watoto hao ambao ni taifa la kesho na kuchangia katika malezi pamoja na kutimiza ndoto zao.
Aidha, alisema watoto hao hawapaswi kutengwa au kuonekana kama wameadhibiwa, bali wanahitaji upendo, malezi na msaada kutoka kwa jamii.
“Tunaamini mavazi haya na chakula tulichowaletea vitasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili watoto hawa, hasa kipindi hiki ambacho kituo kinakabiliwa na upungufu wa chakula. Shule yetu itaendelea kufika mara kwa mara kutoa faraja kwa watoto hawa,” alisema.
Pia aliwasihi watoto wa kituo hicho kuwaheshimu viongozi na walezi wao, pamoja na kujiepusha na makundi mabaya yanayoweza kuharibu maisha yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Ezekiel Mabesa, aliushukuru uongozi wa shule hiyo kwa moyo wa kujitolea na kuomba taasisi nyingine kuiga mfano huo.
“Kama shule tunafahamu ratiba zenu ni ngumu, lakini mmeonyesha upendo na uthubutu kwa kufika hapa kuwafariji watoto wetu,” alisema Mabesa.
Alisema kituo hicho kinahudumia watoto 33 wa kike na wa kiume wenye umri wa kati ya miaka miwili hadi 16, na kuwa wanapatiwa mahitaji yote muhimu ya msingi kama watoto wengine.
“Tunaomba shule na taasisi nyingine zije kutembelea watoto wetu hapa kituoni na kuwapa faraja. Msaada huu umefika wakati muafaka,” alisema.



Hakuna maoni: