Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba amesema kuwa usalama wa nishati umeendelea kuwa sehemu muhimu ya usalama wa taifa kutokana na mchango wake katika kukuza uchumi, utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo ya viwanda.
Amesema changamoto za upatikanaji wa mafuta duniani zimeendelea kuongeza gharama za maisha na kuathiri uchumi wa mataifa mengi ya Afrika, ikiwemo Tanzania, hivyo ni muhimu kwa kila nchi kuwa na vyanzo vya uhakika vya nishati.
Ameeleza hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu athari za mivutano ya kisiasa ya Mashariki ya Kati katika usalama wa nishati katika nchi za Afrika wakati akishiriki Kongamano la 26 linalohusu masuala ya usalama wa nchi (National Security Symposium 2026) linalofanyika jijini Arusha.
Aidha, amebainisha hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha usalama wa nishati nchini, ikiwemo kuimarisha hifadhi ya mafuta ya kimkakati, uwekezaji katika gesi asilia, utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu, pamoja na kuunganisha mifumo ya nishati ya nchi za Afrika.
Kongamano hilo lenye kaulimbiu ya “Sustainable African Development for National Security” limewakutanisha wataalamu wa masuala ya usalama pamoja na washiriki kutoka mataifa mbalimbali kujadili namna ambavyo Afrika inaweza kujenga maendeleo endelevu yanayolinda usalama wa taifa na uchumi wa bara hilo.


Hakuna maoni: