TANESCO KINONDONI KUSINI YAKUTANA NA WATEJA WAKUBWA

Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kinondoni Kusini, Mei 20, 2026, limekutana na kufanya mazungumzo na wateja wakubwa kwa lengo la kuimarisha uhusiano, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka katika maeneo yao ya kazi.

Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini, Adam Abdulla, amesema TANESCO imeamua kukutana na wateja wanaotumia umeme kwa kiwango kikubwa, hususani wa viwanda, hoteli, taasisi za umma na binafsi, ili kuhakikisha wanaendelea kupata huduma bora na ya uhakika ya umeme.

Ameeleza kuwa mkutano huo pia umelenga kuwafahamisha wateja kuhusu maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya umeme pamoja na kusikiliza changamoto wanazokutana nazo ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.

“Tumeamua kufanya mkutano na wateja wetu wakubwa ili kuwapa taarifa sahihi kuhusu ubora wa huduma ya umeme pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maeneo yao ya kazi, kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma zetu,” alisema Mhandisi Adam.

Aidha, amewataka wateja hao kuhakikisha wanalipa bili za umeme kwa wakati, akieleza kuwa hatua hiyo inasaidia kuchochea upatikanaji endelevu wa huduma ya umeme katika maeneo yao.

Kwa upande wao, baadhi ya wateja wameipongeza TANESCO kwa kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme nchini ambapo Mwakilishi wa GIMCO AFRICA, Bw. Sekela Thomas, amesema maboresho hayo yamechangia kuongeza ufanisi wa shughuli za uzalishaji.

“Tunawapongeza sana TANESCO kwa kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini. Hali hii imetuwezesha sisi wateja wakubwa kuendesha shughuli zetu bila vikwazo,” alisema.

Mikutano hiyo ni sehemu ya utaratibu wa TANESCO katika mikoa mbalimbali nchini wa kukutana na makundi tofauti ya wateja kwa lengo la kuimarisha mahusiano, kusikiliza maoni yao na kuwaeleza maboresho yanayoendelea kufanyika kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.