SKA 2026 YAFUNGUA MILANGO YA TUZO ZAIDI YA 40 KWA WAANDISHI NA VYOMBO VYA HABARI

 


Na Mwandishi Wetu.

Waandishi wa Habari na Vyombo vya Habari nchini wanatarajiwa kushindanisha kazi katika zaidi ya tuzo 40 za Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo (Samia Kalamu Awards - SKA) 2026 baada ya waandaaji kuzindua rasmi mchakato wa kupokea kazi zitakazowakutanisha washiriki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza leo Mei 31, 2026 wakati wa uzinduzi wa mchakato wa kupokea kazi za mashindano hayo yanayoandaliwa kwa ushirika kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania -TCRA na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Mwenyekiti wa SKA, Mha. Peter Mwasalyanda, amesema kwa mwaka 2026 washiriki watashindania makundi matatu makuu ambayo ni Tuzo Maalumu za Kitaifa, Tuzo kwa Vyombo vya Habari na Tuzo za Kisekta.

Amesema Kundi la Tuzo Maalumu za Kitaifa linajumuisha Chombo cha Habari Mahiri cha Kitaifa, Mwandishi wa Habari Mahiri na Mwandishi Mahiri wa Nishati Safi ya Kupikia. 

Aidha, Kundi la Tuzo kwa Vyombo vya Habari linajumuisha Magazeti, Televisheni, Redio za Kitaifa, Redio za Kijamii na Chombo cha Habari Mtandaoni.

Tuzo za Kisekta zinahusisha sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Elimu, Afya, Ujenzi, Maji, Nishati, Madini, Diplomasia, Mifugo na Uvuvi, Uchukuzi, Viwanda na Biashara, Utamaduni, Sanaa na Michezo, TEHAMA na Ubunifu.

Nyingine ni Uwekezaji, Vijana, Mazingira, Fedha na Uchumi, Siasa, Uchumi wa Buluu, Sheria, Utawala Bora, Kazi na Ajira, Usalama wa Raia pamoja na sekta nyingine zilizoorodheshwa katika mashindano hayo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amewahamasisha Waandishi wa Habari wote wenye ithibati kushiriki mashindano hayo kwa kuwasilisha kazi zao.

“Wote wanaoshiriki kwenye hizi tuzo wahakikishe wanakuwa na ithibati, wamethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari. Ni muhimu sana kwa sababu ni takwa la kisheria na kitu ambacho hatuwezi kukikwepa. Nawahamasisha tushiriki wote kwa sababu isije ikaonekana ni tuzo za watu fulani tu, kila mmoja awasilishe habari hasa zile ambazo zimezingatia maadili, zimezingatia weledi, lakini pia habari ambazo zina impact (athari Chanya) kwa wananchi,” amesema Kipangula.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, mchakato wa kupokea kazi umeanza rasmi Jumapili Mei 31, 2026 na utaendelea hadi Juni 30, 2026 kupitia tovuti ya samiaawards.tz ambapo Waandishi wa Habari, Vyombo vya Habari na washiriki wa kategoria mbalimbali wanahimizwa kuwasilisha kazi zao kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.