DAR ES SALAAM.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Bw. Tido Mhando, amewataka Waandishi wa Habari nchini kutafakari upya wajibu wao katika kuijenga jamii kupitia maudhui yenye tija, akieleza kuwa ipo haja ya kurejesha hadhi na nguvu ya taaluma hiyo katika kujenga fikra na maendeleo ya taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Bw. Mhando amesema pamoja na JAB kusimamia utoaji wa ithibati kwa kuzingatia vigezo vya elimu na sheria, bado kuna umuhimu wa Waandishi wa Habari kuendelea kujengewa uwezo kupitia mafunzo ya kitaaluma.
“Tukitazama baadhi ya vyombo vyetu vya habari, iwe ni magazeti, redio au televisheni, mambo ya kufikirisha kwa kiasi kikubwa yamepungua. Waandishi wa Habari wanapaswa kutafakari kama hiyo ndiyo taswira wanayotaka kuiacha katika jamii ya Watanzania,” amesema.
Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuunda mtazamo wa jamii, hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha maudhui yanayotolewa yanajenga uelewa, yanakuza maendeleo na yanalinda maslahi ya taifa.
“Tunachosimamia ni kuhakikisha Mwandishi wa Habari anayepata ithibati anakuwa na kiwango cha elimu kisichopungua Diploma, lakini tunataka pia Waandishi wa Habari waendelee kupata mafunzo ili waweze kuimarika zaidi kitaaluma,” amesema.
Amesema ipo haja ya sekta ya habari kutafakari aina ya maudhui yanayopewa kipaumbele, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kujenga fikra na mwelekeo wa jamii.


Hakuna maoni: