Na Mwandishi Wetu,
Dodoma.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), amewaongoza Wabunge kushiriki katika Semina iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kujenga uelewa kwa Wabunge hao kuhusiana na masuala mbalimbali ya uhifadhi na Utalii.
Katika semina hiyo kwa mada mbili zimewasilishwa ikiwa ni pamoja na azma na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa kujenga makumbusho ya Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotarajiwa kujengwa Jijini Dodoma hivi karibuni.
Mada nyingine iliyotolewa kwa Wabunge hao ni kuhusu hatua madhubuti zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na migongano baina ya Wanyamapori wakali na waharibifu dhidi ya binadamu.
Mafunzo hayo yametolewa leo 12 Mei, 2026 Jijini Dodoma na Wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wakiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ambaye amewahakikishia Wabunge hao kuwa licha ya changamoto zilizopo Wizara inachukua hatua mbalimbali na madhubuti za kukabiliana na migongano baina ya binadamu na Wanyamapori wakali na waharibifu kwa kubuni na kutumia teknolojia sambamba na doria zinazofanywa na Askari wa jeshi la uhifadhi
Aidha, Semina hiyo imehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Mwenyekiti wa Kamati Kudumu ya Ardhi Bunge na Maliasili Mhe. Timotheo Paul Mnzava (Mb) Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas, Naibu Katibu Mkuu Nkoba Mabula, Menejimenti ya Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ambapo Wabunge mbalimbali wamepata fursa ya kushauri na kutoa maoni yao.















Hakuna maoni: