WAKULIMA MARA WAPATA TUMAINI JIPYA KUPITIA KILIMO IKOLOJIA, MILIONI 35 ZAWEKEZWA KATIKA UMWAGILIAJI

UFARANSA YATOA MILIONI 35 KUIMARISHA KILIMO IKOLOJIA TARIME.



Na Mwandishi Wetu.

WAKULIMA wilayani Tarime mkoani Mara wanatarajiwa kunufaika zaidi na kilimo cha umwagiliaji baada ya Ubalozi wa Ufaransa kupitia Mradi wa Agro Kilimo unaoratibiwa na Shirika la Island of Peace (IDP), kutoa msaada wa shilingi milioni 35 kwa Kituo cha Maendeleo ya Kilimo na Mazingira cha Mogabiri (MFEC).

Fedha hizo zimetumika kujenga miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi na kusambaza maji kwa ajili ya mashamba ya mfano yanayotumia mbinu za kilimo ikolojia.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kituo hicho mwishoni mwa wiki, Kaimu Meneja wa MFEC, Peter Mwita, alisema msaada huo umeongeza nguvu katika juhudi za kuwawezesha wakulima kutumia kilimo rafiki kwa mazingira na afya ya binadamu.

Alisema kupitia mradi huo, wamefanikiwa kujenga jengo maalum lenye matenki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi lita 20,000 za maji kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji kipindi cha ukame na mvua chache.

“Miundombinu hii inatusaidia kuendesha mashamba darasa mwaka mzima na kuwapa wakulima elimu ya vitendo kuhusu kilimo ikolojia,” alisema Mwita.

Aliongeza kuwa MFEC inaendelea kuhamasisha wakulima kujikita katika kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya mbinu za asili zinazosaidia kuzalisha chakula salama bila kuathiri mazingira.

Mwita alisema kituo hicho kinazalisha mazao mbalimbali kwa mfumo wa kilimo ikolojia yakiwemo migomba, nyanya, hoho, sukuma wiki, viazi, muhogo na kabichi, huku pia kikifuga mifugo kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea ya samadi na mboji.

Aidha alisema kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1986, kimekuwa kikitoa mafunzo ya kutengeneza viuatilifu vya asili kwa wakulima kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Mara.

Kwa mujibu wa Mwita, zaidi ya wakulima 35,000 kutoka vijiji 33 tayari wamefikiwa na elimu hiyo, huku mwitikio ukiendelea kuongezeka kutokana na umuhimu wa kilimo hicho katika kulinda afya na mazingira.

Hata hivyo, alisema bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji mdogo wa rasilimali za asili pamoja na sera ambazo hazijatoa msukumo wa kutosha katika kuhamasisha jamii kutumia kilimo ikolojia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa IDP, Ayesiga Buberwa, alisema Mradi wa Agro Kilimo unalenga kuimarisha mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula kuanzia shambani hadi mezani.

Alisema mradi huo umejikita zaidi katika mafunzo, tafiti na uwezeshaji wa vituo vya kilimo ikolojia ili kuongeza uelewa kwa wakulima na jamii kwa ujumla.

“Tunashukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya kilimo ikolojia ambayo inalenga afya ya binadamu na uhifadhi wa mazingira,” alisema Buberwa.

Alitaja baadhi ya vituo vinavyonufaika na mradi huo kuwa ni pamoja na SJS Mwanga, RECODA, SAT, Bihawana Dodoma pamoja na PPIZ Zanzibar.

Naye Mwakilishi wa Serikali ya Ufaransa, Profesa Jean Luc Paul, alisema nchi hiyo imeendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha sekta ya kilimo tangu mwaka 1980 kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).

Profesa Jean Luc alisema Ufaransa imevutiwa na jitihada za kuendeleza kilimo ikolojia nchini na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta hiyo inaleta mabadiliko chanya kwa wakulima.

“Tunataka kuona kilimo ikolojia kinakuwa suluhisho la uzalishaji wa chakula salama na endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.