DCC BELEKO ARIDHISHWA NA MWITIKIO WA WANANCHI KATIKA BANDA LA TFS WIKI YA MAZINGIRA

Na Mwandishi Wetu, 

Dodoma.

NAIBU Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) anayesimamia Masoko na Matumizi ya Rasilimali za Misitu, DCC Salehe S. Beleko, ameridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wanaotembelea banda la TFS katika Maonesho ya Wiki ya Mazingira yanayoendelea jijini Dodoma, akisema hali hiyo inaonesha kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.

Beleko aliyasema hayo Juni 3, 2026, alipotembelea banda la TFS katika Viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za utoaji elimu kwa wananchi pamoja na maonesho ya bidhaa na huduma zinazotolewa na wakala huo.

Alisema maonesho hayo ni jukwaa muhimu kwa TFS kuonesha mchango wake katika uhifadhi wa mazingira, kukuza uchumi wa kijani na kuhamasisha wananchi kushiriki katika matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.

Katika ziara hiyo, Beleko alitembelea maeneo mbalimbali ya banda hilo na kujionea elimu inayotolewa kuhusu uhifadhi wa misitu, uzalishaji wa miche ya miti, ufugaji nyuki na fursa za uwekezaji zinazotokana na sekta ya misitu.

Pia alikagua mazao na bidhaa mbalimbali zinazotokana na misitu, zikiwemo asali, nta na bidhaa zilizoongezwa thamani, ambazo zimeendelea kuvutia wageni na wadau wanaotembelea maonesho hayo.

Akizungumza na watumishi wa TFS wanaoshiriki maonesho hayo, Beleko aliwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutoa elimu kwa wananchi na kutangaza fursa zilizopo katika sekta ya misitu na nyuki, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia maonesho hayo kufikisha ujumbe wa uhifadhi wa mazingira kwa umma.

Maonesho ya Wiki ya Mazingira yalianza Juni 1 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 5, 2026, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinazoshiriki kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya maliasili.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.