DCEA, VETA KUTOA MAFUNZO KWA WARAIBU WALIOPATA NAFUU

DAR ES SALAAM. 

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) zimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kuwapatia ujuzi waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ili waweze kujitegemea kiuchumi na kuepuka kurejea katika matumizi ya dawa hizo.

Makubaliano hayo yalisainiwa Juni 4, 2026, jijini Dar es Salaam, yakilenga kuimarisha juhudi za urejeshaji wa waraibu katika jamii kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi na stadi za maisha zitakazowawezesha kujiajiri au kupata ajira.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema ushirikiano huo umetokana na kutambua umuhimu wa kuwawezesha waraibu waliopona kupata ujuzi utakaowasaidia kujenga maisha mapya na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha waraibu wanaopata nafuu wanapata fursa za kujitegemea kiuchumi, jambo litakalosaidia kupunguza uwezekano wa kurejea katika matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa upande wake, VETA imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na DCEA katika kutoa mafunzo mbalimbali ya ufundi yatakayowawezesha walengwa kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na shughuli za uzalishaji.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.