Dodoma.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, leo tarehe 2 Juni, 2026 amekutana na Balozi wa Australia nchini Tanzania anayemaliza muda wake wa uwakilishi, Mhe. Jenny Da Rin, kwa mazungumzo ya kumuaga yaliyofanyika jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kiruswa amempongeza Mhe. Jenny Da Rin kwa kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini kwa mafanikio makubwa, huku akitambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Australia, hususan katika maendeleo ya Sekta ya Madini.
Amesema Tanzania na Australia zimeendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo imekuwa na matokeo chanya katika kukuza sekta ya madini na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imeendelea kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya rasilimali madini kwa kuwashirikisha kikamilifu katika shughuli za madini, huku ikitambua mchango wa wawekezaji wa kimataifa, wakiwemo kutoka Australia, katika maendeleo ya sekta hiyo.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na Australia katika maeneo ya utafiti wa madini, uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na maendeleo ya rasilimali watu ili kuongeza uzalishaji na kuifanya sekta ya madini kuwa na tija zaidi kwa Taifa.
“Sekta ya madini inaendelea kukua kwa kasi na inahitaji uwekezaji wa kutosha katika teknolojia, ujuzi na tafiti ili kuongeza uzalishaji na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Kiruswa.
Kwa upande wake, Mhe. Jenny Da Rin ameishukuru Serikali ya Tanzania na Wizara ya Madini kwa ushirikiano mkubwa alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake nchini.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Watanzania kutumia kikamilifu fursa za elimu, mafunzo na semina zinazotolewa na Australia, akibainisha kuwa maarifa na ujuzi unaopatikana kupitia programu hizo unachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta mbalimbali, ikiwemo Sekta ya Madini.
Mhe. Jenny Da Rin ameongeza kuwa moja ya malengo ya ushirikiano kati ya Tanzania na Australia ni kuhamasisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Australia kuja kuwekeza nchini Tanzania pamoja na kuendeleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutatua changamoto zinazoweza kuathiri mazingira ya uwekezaji ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kukuza maendeleo ya nchi hizo mbili.









Hakuna maoni: