GOLDEN VALUE WAPATIWA ELIMU YA NISHATI KATIKA MAONESHO YA WIKI YA MAZINGIRA DUNIANI 2026

Na Mwandishi Wetu,

Meneja wa Shule ya Golden Value Bi. Nuru Nyundo, ameongoza wanafunzi wa darasa la nne na la sita kutembelea banda la Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake katika Maonesho ya Wiki ya Mazingira Duniani 2026 yanayoendelea katika katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma

Ziara hiyo imelenga kuwapatia wanafunzi elimu kuhusu sekta ya nishati na mchango wake katika uhifadhi wa mazingira. 

Wakiwa katika banda hilo, wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu na teknolojia mbalimbali zinazosaidia kupunguza uharibifu wa mazingira.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi. Nyundo amesema kuwa kuwashirikisha wanafunzi katika maonesho hayo ni njia muhimu ya kuwajengea uelewa wa mapema kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kutumia nishati kwa njia endelevu ili kulinda afya na mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, mwanafunzi Maria Yusuph wa darasa la sita amepongeza elimu inayotolewa katika banda la Wizara ya Nishati, akisema imewasaidia kuelewa umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia na namna inavyoweza kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira. Alisema elimu hiyo itamsaidia kuwa balozi wa matumizi ya nishati safi shuleni na nyumbani.

Aidha, wanafunzi hao walitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Nishati na kupata maelezo kutoka kwa wataalamu kuhusu huduma na miradi inayotekelezwa ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi na ya uhakika nchini.

Maonesho ya Wiki ya Mazingira Duniani 2026 yalianza Juni 1 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 5, 2026 jijini Dodoma, yakitoa fursa kwa wananchi, wanafunzi na wadau mbalimbali kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.