FILAMU YA “KIFURUSHI ” YAZINDULIWA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imezindua filamu maalumu ya elimu iitwayo “Kifurushi” ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo, alisema dawa za kulevya zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya za wananchi, usalama wa jamii na maendeleo ya taifa. Alisema athari zake zimechangia kuongezeka kwa uhalifu, kuvunjika kwa familia na kudhoofika kwa nguvu kazi ya taifa, hususan kwa vijana.

Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya, ikiwemo operesheni za ukamataji, utoaji wa tiba kwa waathirika na kampeni za elimu kwa umma.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema tathmini ya mamlaka imebaini kuwa vyombo vya usafiri wa umma hutumika mara kwa mara kusafirisha dawa za kulevya kwa kufichwa katika mizigo na vifurushi visivyojulikana. Kutokana na hali hiyo, DCEA kwa kushirikiana na LATRA na Bodi ya Filamu Tanzania wameandaa filamu hiyo ili kuwapa elimu madereva, makondakta, abiria na wasafirishaji wa mizigo.

Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuepuka kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu, kwani kufanya hivyo kunaweza kuwaingiza katika makosa ya usafirishaji wa dawa za kulevya. Alionya kuwa pale dawa za kulevya zinapokutwa kwenye chombo cha usafiri bila kubainika mmiliki wake, wahudumu wa chombo hicho wanaweza kuwajibishwa kisheria.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania (BASATA), Gelvas Kasiga, alisema filamu ni nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya tabia katika jamii. Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya DCEA na sekta ya filamu utasaidia kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa njia rahisi na yenye ushawishi mkubwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa LATRA pamoja na viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) walieleza kuwa wataendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha vyombo vya usafiri havitumiki katika kusafirisha dawa za kulevya. Wamewataka madereva, makondakta na abiria kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu huo, huku wakisisitiza kaulimbiu ya kampeni hiyo isemayo, “Usafiri Salama Bila Dawa za Kulevya.”

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.