JKCI KUTUA MWANZA, KITUO KIKUBWA CHA MOYO KUJENGWA KANDA YA ZIWA

Wananchi kunufaika, safari za kutafuta matibabu Dar es Salaam na nje ya nchi kupungua.

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza mchakato wa kupanua huduma zake katika Kanda ya Ziwa kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, hatua inayolenga kuanzisha kituo kikubwa cha huduma za moyo kitakachohudumia mamilioni ya wananchi wa ukanda huo.

Mpango huo umejadiliwa katika kikao kifupi kati ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge. Kikao hicho kimejadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa mradi huo muhimu wa afya.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtanda amesema Viongozi wa Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa wanaunga mkono mpango huo na wako tayari kushirikiana na JKCI mara baada ya kupata maelekezo rasmi kutoka Wizara ya Ofisi wa Waziri Mkuu TAMISEMI na Afya.

Amesema uwekezaji huo utapunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu ya moyo, huku ukitoa fursa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Afrika Mashariki kupata huduma za kibingwa karibu zaidi.

Kwa upande wake, Dkt. Kisenge amesema JKCI imeamua kuwekeza Mwanza baada ya kubaini kuwa wagonjwa wengi wanaopata huduma zake hutoka Kanda ya Ziwa na Kaskazini, hivyo kuona umuhimu wa kupeleka huduma karibu na wananchi.

Amesema kituo hicho kitaendeshwa kwa viwango sawa na vya JKCI, ambayo ni miongoni mwa taasisi bora za matibabu ya moyo barani Afrika, na kinatarajiwa pia kuchochea utalii wa tiba kutoka nchi jirani.

Dkt. Kisenge ameongeza kuwa JKCI imejipanga kufanya uchangishaji wa zaidi ya Shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuwasaidia watoto 1,000 wenye matatizo ya moyo, huku sehemu ya fedha hizo ikielekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya huduma za moyo katika Hospitali ya Sekou Toure.

Mbali na matibabu, JKCI itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kinga ya magonjwa ya moyo ili kupunguza idadi ya wagonjwa na kuimarisha afya ya jamii kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.