Na Moshi saidi,
Dar es Salaam.
Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa TAKUKURU Mkoa wa ilala imetoa msaada wa Tshs.mil.20.890 kwa Taasisi ya moyo ya Jakaya kikwete kwa ajili ya kusaidia matibabu ya upasuaji wa moyo kwa watoto.
Akikabidhi hundi hiyo ya fedha kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Crispin Chalamila jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa ilala Faustine Mahijo amesema hiyo kwao ni sehemu ya wajibu wa Taasisi hiyo kusaidia eneo la Afya katika jamii hususani kuokoa maisha ya watoto hao kutokana na kukabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa moyo.
Mahijo amesema mbali ya majukumu yao ya kupambana na kuzuia Rushwa lakini kitendo hicho cha hisani kwa Taasisi hiyo ya moyo ni sehemu yao ya kujitolea katika jamii katika kusaidia kuzipambania afya za watanzania hususani kwa familia zinazopitia changamoto za kumudu gharama za matibabu.
"Mchango wetu huu ukawe ni faraja na ikafungue mlango wa matibabu kwa watoto wetu hawa ili warejee katika afya zao za kawaida na wapone kabisa" amesema Mahijo.
Pia Mahijo amesema msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Dkt.samia suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kupambania afya za mama na mtoto pamoja na watanzania kwa ujumla.
Aidha mkuu huyo wa Takukuru mkoa wa ilala amesifu juhudi za Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya moyo Dkt.Peter kisenge pamoja na jopo lake zima la madaktari Bingwa wa upasuaji kwa namna wanavyopambana katika kuokoa maisha ya watoto wa kitanzania.
Akishukuru msaada huo wa fedha kutoka Takukuru Mkoa wa ilala, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya moyo ya Jakaya kikwete JKCI Dkt.Peter kisenge ameishukuru Takukuru na wafanyakazi wake kwa utu na moyo waliouonesha kwa namna walivyojitoa na kuguswa na changamoto zinazowakabili watoto hao wenye maradhi hayo ya moyo hususani kwa familia zisizo na uwezo kimatibabu.
Dkt.kisenge amesema kutokana na changamoto ya ugonjwa huo wa moyo, wameanzisha kitengo maalum cha Heart team Africa Foundation ambapo amesema moja ya kazi yake ni kukusanya rasilimali fedha utafiti na elimu ili kupata fedha za kusaidia kufanikisha gharama za matibabu ya ugonjwa huo.
Amesema tangu kuanzishwa kwa kitengo hicho wamefanikiwa kukusanya bil.2.7 ambayo imeweza kufanikisha upasuaji na kuokoa maisha ya watoto 305.
Aidha Mkurugenzi mtendaji huyo wa Taasisi ya moyo ameiomba na kuisihi jamii kuendeleea kujitolea kusaidia Taasisi hiyo ili kuweza kufanikisha matibabu ya watoto wanaokabiliwa na maradhi hayo.










Hakuna maoni: